Mahakama ya Russia yaupiga marufuku ufuska wa LGBT, yasema 'umefurutu mpaka'
Mahakama ya Juu ya Russia imelipiga marufuku "vuguvugu la kimataifa la LGBT" na kulitaja kuwa ni kundi lenye "kufurutu mpaka". Uamuzi huo unaathiri pia matawi ya harakati hiyo ya ufuska na mahusiano machafu ya kingono ya watu wa jinsia moja.
Mapema mwezi huu Wizara ya Sheria ya Russia ilifungua mashtaka mahakamani dhidi ya harakati hiyo ikisema, shughuli za "harakati ya LGBT" ni kielelezo cha "kundi lenye msimamo ya kufurutu ada" na hasa kutokana na harakati zake kupanda mbegu za mifarakano ya kidini na kijamii ndani ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la RIA Novosti, kesi hiyo iliyosikilizwa jana Alkhamisi na Mahakama ya Juu ya Russia katika kikao cha faragha ilichukua muda wa masaa manne kabla ya kutolewa hukumu yake.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo, Jaji Oleg Nefedov alisema, "vuguvugu la kimataifa la LGBT" lina misimamo ya kufurutu ada na akatamka rasmi kuwa analipiga marufuku kuendesha shughuli zake katika ardhi ya Russia.
Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, Russia imekuwa ikiongeza hatua kwa hatua makali ya sheria zake zinazolenga kukabiliana na kuenea kwa kile kilichotajwa kama "itikadi ya LGBT."
Kufuatia kutolewa hukumu hiyo inayowatambua rasmi wanaojihusisha na vitendo vya tapo hilo la LGBT kama "wafurutu mipaka" watakaojitangaza kuwa wanajihusisha na liwati, usagaji na kubadilisha jinsia nchini Russia mbali na vitendo vingine vya kundi hilo, wanaweza kuhukumiwa hata kifungo cha miaka mingi jela.
Kanisa la Othodoksi linaloongozwa na Patriarch Kirill, mtu wa karibu na Rais Vladimir Putin limekaribisha hukumu hiyo.
"Ni aina ya kujilinda kimaadili kwa jamii," amesema Vakhtang Kipshidze, afisa wa Kanisa hilo wa mjini Moscow.
Hatua hiyo imepongezwa pia na Chechnya eneo la Shirikisho la Russia ambalo wakazi wake wengi ni Waislamu.
Waziri wa eneo hilo Akhmed Dudaev amesema, Russia imeonyesha kwa mara nyingine tena kwamba si Magharibi kwa ujumla wake wala Marekani itakayoweza kuipokonya nchi hiyo vitu vyake muhimu kuliko vyote ambavyo ni utambulisho wake wa kidini na kitaifa.../