Manuva ya pande tatu ya Korea Kusini, Japan na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i106292-manuva_ya_pande_tatu_ya_korea_kusini_japan_na_marekani
Korea Kusini, Japan na Marekani zimefanya manuva ya pamoja ya anga. Inasemekana kuwa zoezi hilo la kijeshi limefanyika katika kujibu jaribio la kombora la masafa marefu lililofanywa hivi karibuni na Korea Kaskazini katika anga ya Peninsula ya Korea.
(last modified 2023-12-22T09:28:47+00:00 )
Dec 22, 2023 09:28 UTC
  • Manuva ya pande tatu ya Korea Kusini, Japan na Marekani

Korea Kusini, Japan na Marekani zimefanya manuva ya pamoja ya anga. Inasemekana kuwa zoezi hilo la kijeshi limefanyika katika kujibu jaribio la kombora la masafa marefu lililofanywa hivi karibuni na Korea Kaskazini katika anga ya Peninsula ya Korea.

Hata hivyo, nchi hizo tatu karibuni zilianzisha mfumo wa upashanaji taarifa za maonyo ya makombora ya Korea Kaskazini na kuidhinisha mpango wa miaka mingi wa mazoezi ya kijeshi ya pande tatu. Iwapo hatua hizo za Tokyo, Washington na Seoul zinaweza kuzuia shughuli za makombora za Pyongyang au la, wachambuzi wa masuala ya kijeshi na usalama wanatoa jibu hasi kwa sababu Korea Kaskazini inazichukulia hatua hizo za kijeshi za muda mfupi, za kati na za muda mrefu za Marekani na washirika wake kuwa tishio kubwa kwa usalama wake wa kitaifa na hivyo itaendeleza mipango yake ya makombora ili kuimarisha nguvu zake za kukabiliana na tishio hilo.

Kuhusiana na hilo, Ye Wan Ti, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema: "Inaonekana kuwa Marekani inajaribu kuifikisha Peninsula ya Korea kwenye kiwango cha kuchemka na kuisukuma Korea Kaskazini katika kiwango cha kuanzisha mashambulizi ya kijeshi, hatua ambayo itaashiria kumalizika subira yake ya kistratijia dhidi ya Japan na Korea Kusini na hivyo kulitumbukiza eneo hilo katika vita na migogoro." Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo Pyongyang ikawa inatahadharisha dhidi ya vitendo hivyo vya kichochezi vya Marekani na kuonya kuwa huenda vikasababisha mvutano zaidi katika eneo la Asia Mashariki.

Pamoja na hayo nchi hizo zimepuuza maonyo hayo ya Korea Kaskazini na kwa kauli ya Mkuu wa Majeshi ya Pamoja ya Korea Kusini na Marekani yanayojulikana kwa jina la JCS, zimeamua kufanya mazoezi ya kijeshi ya pande tatu kwa kuishirikisha Japan katika eneo la maji ya mashariki mwa Kisiwa cha Kusini cha Jeju, eneo ambalo lina umuhimu mkubwa wa kijeshi kwa Korea Kusini na Japan. Hatua ya Korea Kaskazini kufikia maendeleo makubwa ya kijeshi hasa katika uwanja wa utengenezaji makombora ikiwa chini ya vikwazo vya Marekani na washirika wake, imeitia wasiwasi serikali ya Washington.

Makombora ya Korea Kaskazini

Hii ni kwa sababu kivitendo vikwazo hivyo vimeshindwa kufikia lengo lililokusudiwa. Kwa hiyo, Marekani inatumia kisingizio cha ustawishwaji wa makombora ya Korea Kaskazini kama kisingizio cha kutoa mashinikizo zaidi dhidi ya Pyongyang. Jaribio la hivi karibuni la kombora la balistiki la Korea Kaskazini kwa hakika limevunja mikakati yote iliyowekwa na Marekani na washirika wake kwa ajili ya kusimamisha mpango wa makombora wa Korea Kaskazini na kuthibitisha kwamba nchi hiyo inatumia uwezo wake wote kujiimarisha kijeshi na kwa ajili ya kuzuia mashambulizi ya maadui zake.

Kensuke Takayasu Maba, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema kuhusu suala hilo kwamba: "Japan na Korea Kusini zimeungana na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini, na hivyo kujiweka katika hatari kubwa ya kushambuliwa kwa makombora ya Korea Kaskazini. Kwa hiyo, eneo la Asia Mashariki kabla ya kuwa linahitaji misaada na mazoezi ya kijeshi linahitajia zaidi maelewano na ushirikiano kati ya nchi za eneo hilo ili kutatua matatizo na kuimarisha amani na usalama wa kieneo." Kwa vyovyote vile, kwa mujibu wa Korea Kusini lengo la kufanyika manuva hiyo ya nchi tatu ni kuimarisha uwezo wa nchi hizo latika kujibu kile zinasema ni vitisho vya nyuklia na makombora vya Korea Kaskazini.

Hayo yanajiri katika hali amabyo Pyongyang inaichukulia Marekani kuwa chanzo cha mgogoro katika Peninsula ya Korea, na kuonya mara kadhaa kuhusu matokeo hasi ya mashambulizi ya kijeshi ya Marekani katika eneo hilo. Katika tathmini jumla ya siasa za Marekani katika Peninsula ya Korea, tunaweza kusema kuwa inafuatilia malengo matatu katika eneo hilo, la kwanza likiwa ni kwamba inataka kuchochea ushindani wa nyuklia katika eneo hilo. Pili, Washington inataka kuishinikiza Korea Kaskazini hadi ifikie kiwango cha kumalizika subira yake ya kistratijia na hivyo kuchukua hatua ambayo itainufaisha Marekani, na tatu, ni kuwa inataka kuonyesha kwamba Korea Kaskazini ni tishio la usalama kwa eneo na hivyo kuhalalisha uwepo wake wa kijeshi katika Korea Kusini na Japan, ambapo ina zaidi ya askari 100,000 katika nchi mbili hizo.