Waislamu US wamlaani Biden kwa kuunga mkono maangamizi ya kizazi Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i106418-waislamu_us_wamlaani_biden_kwa_kuunga_mkono_maangamizi_ya_kizazi_gaza
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR) limeijia juu serikali ya Rais Joe Biden wa nchi hiyo kwa kile lilichokitaja kuwa ni 'mchango amilifu' wa Washington kwa mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Dec 25, 2023 08:18 UTC
  • Waislamu US wamlaani Biden kwa kuunga mkono maangamizi ya kizazi Gaza

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR) limeijia juu serikali ya Rais Joe Biden wa nchi hiyo kwa kile lilichokitaja kuwa ni 'mchango amilifu' wa Washington kwa mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Ibrahim Hooper, Mkurugenzi Taifa wa Mawasiliano wa CAIR amesema katika taarifa kuwa, hatua za Biden zitachafua itibari na kupaka matope sura ya Marekani kimataifa hivi sasa na hata katika vizazi kadhaa vijavyo.

Hooper amesema: Ukweli kwamba Rais Biden amekiri kuwa hakutoa mwito wa usitishaji vita katika mazungumzo yake ya karibuni na (Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin) Netanyahu, umeanika dhati ya ukatili ya utawala wake, na mtazamo wake usio wa kiadilifu kwa mauaji ya kimbari Gaza.

Amesema idadi ya kuogofya ya Wapalestina waliouawa huko Gaza inatosha kuwa kithibiti kinachohitajika, ili kutambua ukweli mchungu wa kuwepo mauaji ya kimbari katika eneo hilo la Wapalestina lililo chini ya mzingiro.  

Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani limewataka Wamarekani wa matabaka yote waishinikize serikali ya Biden ichukue hatua za kivitendo za kukomesha chinjachinja, mauaji ya kimbari na mangamizi ya kizazi huko Gaza.

Biden na Netanyahu walifanya mazungumzo ya simu juzi Jumamosi

Taarifa ya kundi hilo linaloongoza kwa kutetea haki za Waislamu nchini Marekani imekuja wakati huu ambapo utawala wa Kizayuni unaendelea kufanya jinai na mauaji ya kinyama Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mapema leo, utawala wa Kizayuni umeua shahidi Wapalestina zaidi ya 70 wakiwemo watoto wadogo na wanawake wajamzito katika shambulizi la anga dhidi ya kambi ya wakimbizi ya al-Maghazi, katikati ya Gaza.

Utawala huo pandikizi ambao umeua shahidi Wapalestina zaidi ya 20,400 huko Gaza tokea Oktoba 7 mpaka sasa, umeshambulia pia mji alikozaliwa Nabii Isa (AS) wa Beit Lahm (Bethlehem), Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, siku hii ambayo mazazi ya Mtume huyo Masih yanaadhimishwa na Wakristo kote duniani. 

Aidha usiku wa kuamkia leo, wanajeshi makatili wa Israel mbali na Bethlehem, walishambulia pia maeneo ya Nablus, Jericho, na Ramallah. Leo asubuhi pia, askari wa Israel wameshambulia mji wa Jenin, ambapo wamewakamata makumi ya vijana wa Kipalestina na kumuua kwa kumpiga risasi kijana Mpalestina aliyekuwa na umri wa miaka 17.