Jan 15, 2024 08:25 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Januari 15

Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyojiri ndani ya siku zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa....

Kombe la Asia; Iran yailaza Palestina

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumapili kama ilivyotarajiwa, iliibuka na ushindi dhidi ya Palestina katika mchuano wa ufunguzi wa fainali za Kombe la Asia. Iran ilifanikiwa kuichabanga Palestina mabao 4-1 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa 'Jiji la Elimu' huko al-Rayyan nchini Qatar. Dalili za Iran kuibuka mshindi zilianza mapema kwa goli la Karim Ansarifard, ambaye alicheka na nyavu dakika 2 tu baada ya kupulizwa kipyenga cha kuanza ngoma. Dakika 10 baadaye, Shojae Khalilzadeh aliongeza la pili kabla ya Mehdi Qayedi kuongeza la 3 dakika chache kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza. Vijana wa Palestina walijitutumua na kufunga la kufutia machozi katika dakika za majeraha kabla ya kwenda mapumzikoni. Iran ililazamisha kabia jahazi la Palestina kupitia goli la kiufundi la Sardar Azmoun, kunako dakikka ya 55 ya mchezo na kuondoka uwanjani na alama 3 safi. Iran sasa inaongoza Kundi C ikiwa na alama 3, sawa na Imarati amabyo ipo katika nafasi ya pili baada ya kuizaba Hong Kong mabao 3-1 mapema Jumapili.

 

Vijana hao wa Kiirani wanaonolewa na Amir Ghalenoei wamepangwa katika Kundi C pamoja na Imarati, Palestina na Hong Kong kwenye michuano hiyo ya kibara iliyong'oa nanga Ijumaa huko Doha. Team Melli ya Iran inapania kuhitimisha ukame wa miaka 47 wa kutwaa taji hilo la kieneo. Michuano hii ya kibara ilipasa kuandaliwa mwaka jana 2023 na China, lakini ikashindikana kutokana na makovu ya janga la Corona. Kabla ya kuana mashindano haya ya kibara yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Asia (AFC), timu hiyo ya kandanda ya Iran iliibamiza Burkina Faso mabao 2-0 katika mchuano wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa mjini Kish, kusini mwa pwani ya Ghuba ya Uajemi hapa nchini, kabla ya kuishukia vibaya Indonesia kwa kuiadhibu mabao 5-0 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa al-Rayyan mjini Doha, Qatar. Iran ilitumia mechi hizo kujiandaa kwa mashindano hayo ya kibara ya kuwania Kombe la Asia.

Ukweaji jabali; Muirani atwaa dhahabu

Mwanamichezo wa Iran, Muhammad Reza Safdarian ametwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya Kombe la Dunia kwenye mchezo wa kukwea jabali na theluji huko Korea Kusini. Safdarian aliibuka kidedea katika fainali ya Jumapili kwenye safu ya wanaume, kwa kukwea jabali bandia la theluji kwa kutumia sekunde 15.34. Raia wa Mongolia, Kherlen Nyamdoo aliibuka wa pili kwa kutumia sekunde 15.99 huku orodha ya tatu bora ikifungwa na mwenyeji Hyeongsub Lim aliyemaliza kwa kutumia sekunde 18.67. Wanamichezo 88 kutoka nchi 16 duniani, wakiwemo 25 kutoka Korea Kusini wameshiriki kwenye mashindano hayo ya kimataifa yaliyofanyika katika mji wa Cheongsong, Korea Kusini, baina ya Januari 12-14. Mashindano hayo ya dunia yameandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Ukweaji Milima na Theluji (UIAA).

Michuano ya AFCON

Duru ya 34 ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON iling'oa nanga Jumamosi nchini Ivory Coast. Michuano hiyo ilipangwa kufanyika mwaka jana 2023, lakini ikaakhirishwa hadi mwaka huu kutokana na msimu wa mvua kubwa iliyonyesha eneo la Afrika Magharibi linakopatikana taifa andalizi la Cote d’Ivoire. Wenyeji Kodivaa wameanza vizuri na kwa mbwembwe mashindano hayo ya kibara, kwa kuisasambua Guinea-Bissau mabao 2-0 katika mchuano wa ufunguzi uliopigwa katika Uwanja wa Alassane Ouattara mjini Abidjan Jumamosi usiku. Mabao ya wenyeji wa mashindano hayo yalifungwa na Seko Fofana kunako dakika ya 4 na Jean-Phillipe Krasso katika dakika ya 58.

Wakati huohuo, bao la mtoka benchi, Garry Rodigues katika dakika za majeraha liliifanya Cape Verde kuambulia ushindi wa kustaajabisha wa mabao 2-1 dhidi ya miamba ya soka barani Afrika, Ghana siku ya Jumapili mjini Abidjan.

Kabla ya hapo, Misri na Msumbiji zilitoa sare ya mabao 2-2 kwenye mchuano mwngine wa Kundi B. Mkwaju wa penati uliopigwa na mshambuliaji nyota wa Liverpool, Muhammad Salah uliwafanya Mafarao waponee kwenye mchuano huo.

 

Fowadi wa Nigeria, Victor Osimwe ambaye karibuni alitawazwa kuwa Mchezi Bora wa Soka Barani Afrika, aliipa timu yake bao la kusawazisha ilipovaana na Equatorial Guinea kwenye mchuano wa Kundi A Jumapili. Mechi hizo zinasakatwa katika viwanja vya miji ya Abidjan, Yamoussoukro, Bouake, San Pedro, na Korhogo kati ya Januari 13 na Februari 11, 2024. Mwakiilishi wa Afrika Mashariki kwenye mashindano hayo, Taifa Stars ya Tanzania imeapa kupambana kufa kupona kwenye mashindano hayo.

Nchi 24 za Afrika zinapambania Dola milioni 17 za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa timu ambayo itatwaa ubingwa wa AFCON kwenye fainali itakayopigwa Februari 11.

Fainali ya Mapinduzi Cup; Mlandege Hoyee!

Klabu ya Mlandege ya Unguja visiwani Zanzibar siku ya Jumamosi ilishuka dimbani kuvaana na miamba ya soka Tanzania, klabu ya Simba katika fainali ya Kombe la Mapinduzi. Mlandege FC imefanikiwa kuutetea ubingwa wake mara baada ya kuichapa Simba Sc bao 1-0 kwenye fainali ya michuano ya Mapinduzi Cup ambayo ilikuwa inaendelea visiwani Zanzibar. Katika mchezo huo ambao Simba Sc ilifanikiwa kuutawala mchezo kwenye vipindi vyote licha ya kutofanikiwa kupata bao huku wakiruhusu kufungwa bao moja na kushindwa kunyakua taji hilo. Bao pekee ambalo limewafanya Mlandege Fc kuibuka washindi limefungwa na Joseph Akandwanao mnamo dakika ya 54 ya mchezo baada ya kuwatoka mabeki wa Simba Sc na kupiga shuti kali lililomshinda kipa na kuingia nyavuni. Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi ndiye aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mchezo huo akitinga uwanjani mapema tu dakika 25 kabla ya mchezo kuanza, pia akiwemo makamu wake wa pili Hemed Suleiman na viongozi wengine wa serikali ya Bara na Zanzibar.

Mchezaji bora wa Mashindano: Fabice Ngoma (Simba) Kipa Bora wa Athuman Hassan (Mlandege). Mfungaji Bora: Elvis Rupia wa Singida Fountain Gate. Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amewasihi mashabiki wa klabu hiyo kutokuwa wanyonge kwa kulikosa Kombe la Mapinduzi, kwani wamefaidika zaidi na michuano hiyo kuliko vile walivyopoteza. Ally amesema hayo alipowasili katika Bandari ya Jiji la Dar es Salaam, akitokea visiwani Zanzibar na kikosi cha Simba kushiriki Michuano ya 18 ya Mapinduzi.

Dondoo za Hapa na Pale

Afrika Kusini imemvua David Teeger majukumu yake kama nahodha wa Kombe la Dunia lijalo la Kriketi kufuatia matamshi yake ya kuunga mkono jinai za utawala haramu wa Israel. Siku ya Ijumaa, Shirikisho la Kriketi ya Afrika Kusini (CSA) ilitangaza uamuzi wa kumshusha cheo Teeger kama Nahodha wa timu ya Afrika Kusini ya chini ya umri wa miaka 19 kwa ajili ya hatua za usalama na usalama baada ya hotuba yake katika tuzo za Jewish Achiever Awards. Teeger alitazamiwa kuiongoza Afrika Kusini katika mashindano ya Kombe la Dunia ya Kriketi ya Vijana wasiozidi umri wa miaka 19, yatakayoanza Januari 19.

CSA ilisema kwenye taarifa kwamba katika hali zote, imeamua David aondolewe unahodha wa mashindano hayo. "Hili ni kwa manufaa ya wachezaji wote, timu na David mwenyewe,” imesema taarifa hiyo. Teeger aliripotiwa kusema kwamba tuzo aliyopokea mnamo Oktoba ataitunuku jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel Makundi kadhaa yalikuwa yamewasilisha malalamiko juu ya maoni ya Teeger na baada ya hapo alikuwa chini ya uchunguzi.

David Teeger aliyevuliwa unahodha

 

Na wanariadha wa Kenya Hellen Obiri na Wesley Kiptoo wameridhika na nafasi za pili kwenye mbio za Houston Half Marathon nchini Amerika, Jumapili, Janauri 14, 2024. Bingwa wa Boston na New York Marathon Obiri anayejiandaa kutetea taji la Boston Marathon hapo Aprili 15, 2024 amekamilisha mbio hizo za kilomita 21 kwa saa 1:06:07, katikati ya Waethiopia Sutume Kebede (1:04:37) na Buze Kejela (1:06:24). Kiptoo alikamata nafasi ya pili kwa upande wa wanaume kwa 1:00:43, akimaliza katikati ya Waethiopia Jemal Yimer (1:00:42) na Milkesa Tolosa (1:00:45). Naye Vicoty Chepng’eno ameridhika na nafasi ya pili katika mbio za Houston Marathon kwa saa 2:19:55, katikati ya Waethiopia Rahma Tusa (2:19:33) na Melesech Beyene (2:24:50).

…...........MWISHO....…..

 

Tags