IAEA; chombo cha mashinikizo ya Magharibi dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i107442-iaea_chombo_cha_mashinikizo_ya_magharibi_dhidi_ya_iran
Nchi za Magharibi zinaendelea kutoa mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Iran kupitia Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa IAEA katika wakati ambapo Jamhuri ya Kiislamu inashirikiana kikamilifu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hata nje ya majukumu yake.
(last modified 2024-01-20T23:07:26+00:00 )
Jan 20, 2024 23:07 UTC
  • IAEA; chombo cha mashinikizo ya Magharibi dhidi ya Iran

Nchi za Magharibi zinaendelea kutoa mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Iran kupitia Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa IAEA katika wakati ambapo Jamhuri ya Kiislamu inashirikiana kikamilifu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hata nje ya majukumu yake.

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, alidai katika  matamshi yake ya kisiasa yaliyoko nje ya wadhifa wake,  kuwa  ushirikiano kati ya Iran na wakala huo umetekwa kutokana na mzozo kati ya Iran na nchi za Magharibi. Grossi alidai katika mahojiano  aliyofanya pambizoni mwa mkutano wa Davos kuwa: "Iran imewakataa  baadhi ya wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kutokana na uraia wao. Hii ni njia ya kutuadhibu kutokana na matukio yasiyohusiana na IAEA. Wakati Ufaransa, Uingereza au Marekani zinapofanya jambo wasilolipenda Iran,  IAEA inakuwa wa mhanga  wa mizozo baina yao. Jambo hili halikubaliki kwa upande wetu."

Tab'an hii si mara ya kwanza kwa Mkurungezi Mkuu wa IAEA shirika hilo anaishutumu kisiasa Iran. Hivi karibuni pia na baada ya kusimamishwa kibali cha baadhi ya wakaguzi wa shirika hilo nchini Iran, Grossi alidai kuwa hatua hiyo inaathiri shughuli za kawaida za wakala huo. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na  katika safari  ya siku mbili ya Grossi hapa mjini Tehran mwezi Machi 2023 ilikubali kwa hiari kufanyika uhakiki na ufuatiliaji zaidi wa shughuli za wakaguzi wa wakala huo, ndani ya mfumo wa sheria ya kimkakati ya Bunge (Sheria ya Hatua ya Kimkakati ya Kuondoa Vikwazo na Kulinda Maslahi ya Taifa la Iran).

Hii ni katika hali ambayo dhima za kisheria za nchi wanachama wa wakala wa IAEA kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa inatofautiana na majukumu yanayokubaliwa kwa hiari na nchi kama vile Iran. Kadhalika, licha ya Marekani kujitoa katika JCPOA kinyume cha sheria na Washington kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya mapatano ya JCPOA, lakini pamoja na yote hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali kwa hiari yake kufanyika uhakiki na ufuatiliaji wa shughuli zake za nyuklia kama yanavyosema mapatano ya JCPOA.

Kwa kuzingatia hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na kupinga madai hayo, imekuwa ikisisitiza mara kwamba kuwa kuna mipaka ya majukumu kwa kila nchi wanachama wa IAEA.

Madai ya hivi karibuni ya Grossi yanahusu kusimamisha Iran vibali vya wakaguzi wanane wa IAEA  mwezi Septemba mwaka jana, wakati hatua hiyo ilichukuliwa kwa mujibu wa  Kifungu cha 9 cha Makubaliano ya pamoja kati ya Iran na IAEA, na kwamba Tehran ina haki ya kutoidhinisha vibali vya  baadhi ya wakaguzi wa wakala huo.  Ikumbukwe pia kwamba hivi sasa wakaguzi 117 wameteuliwa mahsusi kwa ajili ya Iran, hivyo Grossi hapaswi kubana utekelezaji wa majukumu ya wakala huo kwa ajili ya wakaguzi wachache tu. 

Makao makuu ya IAEA

Ni wazi kwamba, kurudiwa  madai na mitazamo ya kisiasa ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala dhidi ya Iran kunaimarisha dhana kwamba wakala huo unatoa mashinikizo dhidi ya Tehran nje ya majukumu yake ya kisheria, ili  kuilazimisha ikubali kutwishwa na kubebeshwa makubaliano wanayotaka Wamagharibi.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki unapaswa kufuata sheria na kufanya kazi kiutaalamu unaposhughulikia mradi wa nyuklia wa Iran ambao ni wa amani kikamilifu na usikubali kutumiwa na nchi za Magharibi kama chombo cha kutoa mashinikizo ya  kisiasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, alisema kuhusiana na jambo hilo kwamba, Grossi,ametoa madai ambayo hutolewa mara kwa mara na Marekani na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani bila ya kuzingatia sheria zilizoainishwa katika Makubaliano ya Kinga ya Ulinzi,  Mbali na hilo, madai hayo ya Grossi yako nje kabisa ya majukumu ya Iran. Kuendelea siasa hizo za  Mkurugenzi Mkuu wa IAEA si tu kunatia doa itibari ya wakala huo bali kunaharibu pia ushirikiano uliojengeka kwa miaka mingi kati ya IAEA na nchi mwanachama ambayo inatekeleza kikamilifu majukumu yake yote.