Walimwengu wailaani US kwa kutumia veto kuzuia usitishaji vita Gaza
(last modified Wed, 21 Feb 2024 02:57:12 GMT )
Feb 21, 2024 02:57 UTC
  • Walimwengu wailaani US kwa kutumia veto kuzuia usitishaji vita Gaza

Mataifa na mashirika mbali mbali ya kimataifa yamelaani vikali hatua ya Marekani ya kutumia kura yake ya turufu kupinga rasimu ya azimio iliyowasilishwa na Algeria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, la kutaka kusitishwa mara moja mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani (CAIR) limesema hatua ya Marekani ya kukataa kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza kwa kulipigia kura ya veto azimio hilo ni ya fedheha, huku likimtaka Rais Joe Biden aache kujifanya kuwa wakili mtetezi wa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel.

Mkurugenzi Mkuu wa CAIR, Nihad Awad amenukuliwa na kanali ya al-Jazeera akisema kuwa, kitendo hicho cha US kwa mara nyingine tena kimeonyesha ushiriki kamili wa Washington katika jinai na uhalifu unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel.

Katika kikao hicho cha jana, wawakilishi wa nchi 13 kati ya 15 wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walipiga kura kuunga mkono azimio hilo la kusitishwa vita Ukanda wa Gaza. Marekani ilipiga kura ya veto dhidi ya azimio hilo huku mshirika wake, Uingereza, ikijizuia kupiga kura.

Hii ni mara ya tatu kwa Marekani kutumia kura yake ya veto katika Baraza la Usalama kupinga azimio la kusitishwa vita vya maangamizi ya kizazi vinavyoendelea kufanya na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza tokea Oktoba 7, 2023.

Jason Lee, Mkurugenzi wa shirika la misaada ya kibinadamu la Save the Children katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amelaani hatua hiyo ya US na kusema kuwa, taasisi hiyo imeshtushwa na hatua hii mpya ya kutamausha ambayo inaashiria kufeli kwa jamii ya kimataifa. 

Kabla ya kikao cha jana, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield alisema katika taarifa kuwa, muswada huo utaangushwa na Marekani katika Baraza la Usalama eti kwa kuwa "Matini (ya rasimu hiyo) inaweka hatarini mazungumzo hasasi ya usitishaji vita."

Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour amesema, "Ujumbe uliotolewa leo (jana) kwa Israel kwa veto hii ni kwamba, (Israel) ina kibali cha kuendelea kufanya mauaji bila kuwajibishwa."

Naye Balozi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa, Amar Bendjama amesema kupinga azimio la usitishaji vita katika Baraza la Usalama kumetoa kibali cha kutumia njaa kama silaha ya vita; na kwamba kuna udharura wa kutekelezwa usitishaji vita katika ukanda huo haraka iwezekanavyo.

Marekani imetumia turufu yake kupinga usitishaji vita Gaza katika hali ambayo, Wapalestina karibu 30,000 wameuawa shahidi hadi sasa katika mashambulizi ya kikatili ya Israel tokea Okotba 7, 2023; huku wengine zaidi ya elfu 69 wakijeruhiwa.