Feb 28, 2024 06:48 UTC
  • Waingereza waitaka London iache kuipa silaha Israel

Wanaharakati wa haki nchini Uingereza wamefanya maandamano makubwa ya kuitaka serikali ya nchi hiyo isitishe mauzo ya silaha kwa utawala haramu wa Israel.

Wanaharakati hao waliokusanyika nje ya Uwanja wa Twickenham mjini London, palipokuwa panafanyika Maonyesho ya Silaha, mbali na kutaka kutoruhusiwa Israel kushiriki kwenye maonyesho hayo, lakini pia wametaka hatua ya kuipelekea silaha Israel ikomeshwe mara moja.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, waandamanaji hao wamesema upelekaji wowote wa silaha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zitatumika katika mashambulizi ya ardhini na angani dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa unakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu, na lazima ukomeshwe.

Kadhalika waandamanaji hao mjini London wamelaani na kupinga jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza, huku pia wakitaka kukomeshwa mfumo wa ubaguzi wa apartheid wa utawala huo haramu. 

Maandamano ya Uingereza ya kuwaunga mkono raia wa Ukanda wa Gaza yamekuwa harakati ya kisiasa licha ya mashinikizo na vizuizi vya serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya kuwanyamazisha waungaji mkono wa Palestina. 

Siku chache zilizopita, Waziri Kiongozi wa Scotland, Humza Yousaf aliitaka Serikali ya Uingereza kusitisha uuzaji wa silaha kwa utawala wa Israel kutokana na utawala huo wa Kizayuni kuendeleza mauaji ya kimbari ya raia Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Alisema jinai zimeshuhudiwa katika vita vya Gaza ikiwa ni pamoja na raia wasio na hatia wanaopeperusha bendera nyeupe kuuawa kwa kupigwa risasi, ulipuaji wa kambi za wakimbizi na ulipuaji wa shule.

Nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikiyataka madola ya Magharibi yaache kutuma silaha na zana za kijeshi kwa utawala unaofanya mauaji ya kimbari wa Israel.

 

Tags