Mar 07, 2024 12:04 UTC
  • China yaunga mkono Palestina kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesema nchi yake inaunga mkono Palestina kupewa uanachama "kamili" wa Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa takwa la muda mrefu la watu wa Palestina la kuanzisha nchi yao huru haliwezi kuepukika tena.

"Tunaunga mkono Palestina kuwa mwanachama rasmi wa Umoja wa Mataifa," amesema Wang Yi katika mkutano na waandishi wa habari.
 
Wang amebainisha kuwa, maafa ya Ghaza kwa mara nyingine tena yameukumbusha ulimwengu kwamba ukweli kuwa maeneo ya Palestina yamekaliwa kwa mabavu kwa muda mrefu hauwezi tena kupuuzwa.
 
Ameongeza kuwa, takwa la muda mrefu la watu wa Palestina la kuanzisha nchi huru haliwezi kuepukika tena, na dhulma ya kihistoria wanayopata watu wa Palestina haiwezi kuendelea kwa vizazi bila ya kurekebishwa.

Beijing imekuwa ikitoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano tangu utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulipoanzisha vita vya sasa vya kikatili na mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Ghaza Oktoba 7 mwaka jana.

Kihistoria, China imekuwa ikiunga mkono suala la Palestina na kuunga mkono suluhisho la mataifa mawili kwa mzozo wa Israel na Palestina.
 
Rais wa nchi hiyo Xi Jinping ametoa wito wa kufanyika "mkutano wa kimataifa wa amani" ili kutatua mzozo huo.
 
Vita vya Israel dhidi ya Wapalestina waliozingirwa wa Ghaza vimeingia katika siku yake ya 153, vikiwa vimeshaua watu wasiopungua 30,717, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, na kujeruhi 72,156, huku ripoti mpya ikifichua kuwa tangu Oktoba 2023 Marekani iliidhinisha mauzo ya silaha zaidi ya 100 kwa utawala huo wa Kizayuni.../ 

Tags