Mar 27, 2024 02:07 UTC
  • Moscow: EU imekiri kuwa inahudumia ubeberu wa Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema matamshi ya karibuni ya Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ni ungamo la Magharibi kwamba inajihusisha na mgogoro wa Ukraine ili kuisaidia Marekani kudumisha nafasi yake ya ubeberu duniani.

Maria Zakharova amesema kauli ya Borrell haina mfungamano wowote na kile kinachodaiwa na Wamagharibi kuwa ni upendo kwa Waukraine, bali imeashiria wazi kuwa nchi za Ulaya ni mwanasesere wa kuhudumia uchu wa Marekani wa kudumisha ubeberu wake duniani, na nafasi yake inayoporomoka kwa kasi katika masuala ya kimataifa.

Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CNN hivi karibuni, Borrell alidai kuwa, "EU haiwezi kuruhusu Russia ishinde vita hivi (dhidi ya Ukraine), vinginevyo maslahi ya Marekani na Ulaya yatasambaratishwa."

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa EU

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Ulaya aliendelea kusema: Magharibi haiiungi mkono Kiev kutokana na ukarimu au kwa kuwa inalipenda sana taifa la Ukraine, lakini (inafanya hivyo) kwa maslahi yenyewe, na pia kwa maslahi ya Marekani kama mchezaji wa kilimwengu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amejibu kauli hiyo ya Borrell kwa kusema: Hii ni mara ya kwanza kwa mwakilishi wa tawala za Magharibi kuzungumza bayana kuhusu chimubuko halisi la mgogoro wa Moscow na Kiev.

Zakharova ameongeza kwa kusema, kwa upande mmoja nchi za Magharibi zinashinda kutuma silaha Ukraine, na kwa upande wa pili zinadai kwamba zinafanya juhudi za kupatia ufumbuzi mgogoro wa Moscow na Kiev.

Tags