May 04, 2024 06:57 UTC
  • Watoto wa Gaza
    Watoto wa Gaza

Wabunge wa chama cha Democratic cha Marekani wamesema katika barua waliyomwandikia Rais Joe Biden wa nchi hiyo kwamba wanaamini kuna ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha kwamba Israel imekiuka sheria za Marekani kwa kuzuia mtiririko wa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Ukanda wa Gaza unaoendelea kushambuliwa kinyama na jeshi la utawala wa Kizayuni.

Barua hiyo, iliyotiwa saini na wajumbe 86 wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, imesema kwamba vikwazo vilivyowekwa na Israel juu ya misaada "vinazua shaka" juu ya kukiukwa kifungu cha Sheria ya Msaada wa Kigeni wa Marekani ambacho kinawataka wanaopokea silaha zinazofadhiliwa na Marekani kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kuruhusu mtiririko huru wa misaada.

Wabunge hao wa Kongresi wamesema kuwa serikali ya Israel imekataa maombi ya mara kwa mara ya Marekani ya kutaka kufungua njia za baharini na nchi kavu ili kupeleka misaada huko Gaza. Wameashiria ripoti inayosisitiza kwamba, Israel imezuia kupelekwa chakula cha kutosha ili kuepusha njaa kwa watu wa Gaza, na imeweka mfumo wa ukaguzi na vizuizi dhidi ya misaada, suala ambalo limezuia usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza.

Israel inafanya mauaji ya kimbari Gaza

Jumuiya na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanaituhumu Israel, inayokingiwa kifua na Marekani, kwamba inatumia njaa kama silaha ya vita dhidi ya watu wa Gaza. 

Awali, shirika lisilo la kiserikali la Oxfam liliishutumu Israel kwa kuzuia kuingia kwa misaada ya kibinadamu "makusudi" katikak Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na chakula na vifaa vya matibabu, kinyume na sheria ya kimataifa ya kibinadamu.