Ireland kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland amesema kuwa, mnamo siku chache zijazo, Dublin itaitambua rasmi nchi huru ya Palestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la (IRNA) Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland Mike Martin ametangaza kuwa nchi yake itaitambua nchi huru ya Palestina kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Mei.
Kabla ya hapo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ireland alikaribisha kupitishwa azimio la kuunga mkono kupatiwa uanachama kamili Palestina katika Umoja wa Mataifa na kusema kuwa wakati umefika wa kuainishwa hatima ya watu wa nchi hiyo.
Azimio lililopendekezwa na nchi za Kundi la Kiarabu kuhusu uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa liliidhinishwa siku ya Ijumaa ya tarehe 10 Mei katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kura 143 zilizounga mkono.
Azimio hilo linaipa Palestina haki na mapendeleo maalum na kulitaka Baraza la Usalama lipitie upya kwa mtazamo chanya ombi la taifa la Palestina la kuwa mwanachama wa 194 wa Umoja wa Mataifa.
Kwa sasa Palestina si mtazamaji asiye mwanachama na imekuwa ikijaribu kwa miaka mingi kuwa mwanachama kamili wa chombo hicho cha kimataifa.
Juhudi hizo za Palestina zilipingwa na Marekani kwa kura ya veto mnamo mwezi uliopita katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kwa kupitishwa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Palestina imetambuliwa kama nchi inayostahiki kuwa mwanachama kamili.
Nchi za Uhispania, Malta na Slovenia pia zilitangaza hapo kabla kwamba zinakusudia hadi ifikapo Mei 21 ziwe zimeitambua nchi huru ya Palestina. Hadi sasa nchi 141 zimeshaitambua nchi ya Palestina.
Wakati huo huo Rais Michael D. Higgins wa Jamhuri wa Ireland, amelaani vikali kitendo cha walowezi wa Kizayuni cha kuishambulia misafara ya misaada ya kibinadamu inayopelekwa Ukanda wa Gaza na kusema kuwa mashambulizi hayo yanafanyika wakati Wapalestina wa Gaza wanateseka kwa njaa.
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni viliripoti jana kuwa walowezi wameshambulia malori yaliyokuwa yamebeba misaada ya kibinadamu karibu na Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu.
Rais wa Ireland aidha amesema wafanyakazi wanaopeleka misaada huko ukanda wa Gaza hivi sasa wanakabiliwa na hali mbaya na ya kutisha na kuongeza kuwa katika mji wa Rafah siku ya Jumatatu gari lililokuwa na alama inayoonekana wazi ya Umoja wa Mataifa (UN) lilipigwa risasi na Wazayuni na mmoja wa wafanyakazi aliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Zaidi ya Wapalestina elfu 35 wameuawa shahidi na wengine elfu 79 wamejeruhiwa tangu yalipoanza mashambulizi ya majeshi ya Israel huko ukanda wa Gaza Oktoba 7 2023.