Le Monde: Ususiaji waziathiri vibaya bidhaa za Marekani
(last modified Fri, 14 Jun 2024 13:29:23 GMT )
Jun 14, 2024 13:29 UTC
  • Le Monde: Ususiaji waziathiri vibaya bidhaa za Marekani

Gazeti la Le Monde la Ufaransa limeripoti kwamba makampuni ya Marekani yako katika kipindi kigumu hivi sasa kwa kususiwa bidhaa zao kutokana na uungaji mkono wao kwa Israel.

Katika toleo lake la jana, gazeti hilo maarufu la Ufaransa limeandika kuwa: Viongozi wa masuala ya biashara katika eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) hawana furaha na wana wasiwasi kuhusu madhara ya muda mrefu ya kiuchumi yanayotokana na msaada wa Marekani kwa Israel katika vita vya Ghaza.

Gazeti la Le Monde la Ufaransa limeripoti kuwa, makampuni ya Marekani yanaendelea kupata hasara na yana wakati mgumu kwa kususiwa bidhaa zake kutokana na kuunga mkono jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

Gazeti hilo la Le Monde la Ufaransa pia limeandika kwamba mikahawa ya Starbucks na ya McDonald huko Mashariki ya Kati si tu imesusiwa vibaya na wateja, lakini pia mapato yao ya robo mwaka yanaonyesha kupungua mauzo, na hili linathibitisha kwamba kampeni ya kuyasusia makampuni ambayo yanatuhumiwa kuuunga mkono utawala wa Kizayuni inafanya kazi na ni chungu kwa Israel na Marekani.

Ripoti ya gazeti hilo iliyoandikwa na mwandishi wake wa mjini Beirut, Helen Salon, imesema pia kuwa, kundi hilo la makampuni yanayotuhumiwa kuiunga mkono Israel linapata hasara kutokana na kampeni ya kuhamasisha watumiaji wasusie bidhaa za makampuni ya kundi hilo; kampeni ambayo hivi sasa ni maarufu sana katika eneo la Asia Magharibi.

Gazeti hilo la nchini Ufaransa aidha limesema kuwa, kundi la Al-Shaya ambalo linafanya kazi katika sekta ya bidhaa za rejareja kwenye nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na ni mmiliki wa Starbucks kanda ya Asia Magharibi, linafikiria kupunguza wafanyakazi zaidi ya elfu mbili kutokana na matokeo mabaya ya kususiwa bidhaa zake kwa sababu ya vita vya Ghaza.