Oxfam yaikosoa serikali ya London kwa kuendelea kutuma silaha Israel
(last modified Tue, 18 Jun 2024 05:40:43 GMT )
Jun 18, 2024 05:40 UTC
  • Oxfam yaikosoa serikali ya London kwa kuendelea kutuma silaha Israel

Shirika la kimataifa la misaada la Oxfam limelaani siasa za serikali ya Uingereza za kuuzia silaha utawala haramu wa Israel, ilihali inajua fika kwamba silaha hizo zinatumika katika kuwaua maelfu ya watoto wasio na hatia wa Kipalestina huko Ghaza.

Kwa mujibu wa takwimu za karibuni za Wizara ya Afya ya Gaza, idadi ya mashahidi wa vita vya Israel dhidi ya Gaza tangu Oktoba 7, 2023 imefikia watu 37,232 na idadi ya waliojeruhiwa 85, 037. Mkuu wa Oxfam yenye makao makuu yake nchini Uingereza, amelaani vikali siasa hizo za serikali ya London kuhusu uuzaji wa silaha kwa Israel, na kutangaza kuwa shirika hilo linajiandaa kufungua kesi mahakamani dhidi ya siasa hizo za serikali ya London.

Awali, katika barua ya wazi iliyowaandikia Mawaziri wa Biashara na Mambo ya Nje wa Uingereza, na kwa kuzingatia idadi kubwa ya mashahidi na majeruhi wa vita vya Gaza, Oxfam ilitahadharisha kuwa serikali ya London inahusika katika maafa ya kibinadamu katika ukanda huo kwa kuuunga mkono utawala wa Kizayuni na kuupa silaha unazotumia kufanya mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina.

Jumamosi iliyopita watetezi wapatao 150,000 wa Palestina waliandamana katika mitaa ya jiji la London wakipeperusha bendera za Palestina, na kutaka kutekelezwa mara moja maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ na ya Jinai ICC kuhusu vita vya Gaza na kutiwa mbaroni watawala wa Israel wanaoendelea kufanya jinai za kutisha dhidi ya raia wa kawaida wa Palestina na hasa watoto na wanawake, na wakati huo huo kusisitiza haja ya kupigwa marufuku mauzo ya silaha za Uingereza kwa utawala wa Kizayuni na vile vile kufukuzwa nchini humo balozi wa Israel.

Takwimu za serikali ya Uingereza zinaonyesha kuwa kuanzia tarehe 7 Oktoba hadi Mei 31, Uingereza ilitoa leseni 108 za kuuziwa silaha Israel,  ambapo 37 kati ya hizo ziliainishwa kama za "kijeshi" na 63 za "kiraia".

Shirika la Oxfam

Wizara ya Biashara ya Uingereza katika ripoti yake ambayo nakala yake ilichapishwa karibuni kwenye tovuti ya serikali ya nchi hiyo, imeorodhesha nyaraka zinazohusiana na mauzo ya silaha kwa utawala wa Kizayuni katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja uliopita.

Ripoti hiyo imechapishwa baada ya wabunge wa Uingereza kuitaka serikali ifafanue kuhusu upelekaji wa silaha kwa utawala wa Kizayuni. Kufuatia kutolewa vibali hivyo, mashirika yanayounga mkono haki za binadamu za Wapalestina, zikiwemo Taasisi ya Al-Haq na Global Legal Action Network, yaliwasilisha kesi mahakamani kuhusu udharura wa kuchunguzwa mauzo ya silaha za Uingereza kwa Israel, ambapo Oxfam nayo imesema tayari imepata kibali cha kujiunga na kesi hiyo.

Kwa mujibu wa kura za uchunguzi wa maoni, wengi wa wananchi wa Uingereza wanataka kupigwa marufuku mauzo ya silaha kwa utawala wa Kizayuni na kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza. Matokeo ya Taasisi mashuhuri ya YouGov yanaashiria kuwa, asilimia 56 ya Waingereza wanataka serikali ya nchi hiyo isitishe utoaji leseni za kutuma silaha kwa utawala wa Kizayuni katika kipindi chote cha vita huko Gaza. Makumi ya wabunge wa Uingereza pia wametoa ombi kama hilo katika barua mbili tofauti kwa David Cameron, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo.

Pia, Chama cha Taifa cha Scotland na cha Liberal Democrats na vilevile Mshauri wa zamani wa Usalama wa Kitaifa wa Uingereza ni miongoni mwa vyama na watu ambao wametaka kusimamishwa mara moja utoaji wa leseni za uuzaji wa silaha kwa Israeli. Chama cha Labour, kikiwa ni chama cha pili kwa ukubwa nchini Uingereza, pia kinasema kwamba ikiwa mawakili wa serikali wanaamini kuwa utawala wa Israel umekiuka sheria za kimataifa, basi uuzaji wa silaha kwa utawala huo unapaswa kukomeshwa.

Licha ya upinzani huo mkubwa wa ndani, lakini hakuna mabadiliko yoyote yanayoonekana katika mwenendo wa serikali ya London katika kuegemea upande wa serikali ya Netanyahu inayopinga amani na kutekeleza jinai za kutisha dhidi ya watu wa Gaza. Serikali ya Uingereza, mbali na kuuzia silaha utawala haramu wa Israel, imetuma jeshi lake la wanamaji kusaidiana na Marekani katika kulinda meli zinazotuma silaha na bidhaa nyinginezo kwa utawala wa Israel na wakati huo huo kukabiliana na Jeshi la Wananchi wa Yemen linalojaribu kuzuia meli hizo kufika katika bandari za ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, ikiwa ni katika mchango wake wa kuunga mkono wananchi madhlumu wa Palestina.