Jul 16, 2016 03:53 UTC
  • Jaribio la Mapinduzi ya Kijeshi Uturuki, Rais Erdogan Aapa kuwaadhibu wahusika

Kumejiri jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini Uturuki Ijumaa usiku huku watu 42 wakiripotiwa kupoteza maisha katika mji mkuu Ankara na Rais ReccepTayyib Erdogan akisema jaribio hilo limeshindwa.

Ijumaa usiku kundi moja la Jeshi la Uturuki lilisema limechukua udhibiti kamili wa nchi na kwamba Rais Erdogan na Waziri Mkuu Binali Yildirim wameondolewa madarakani.

Kulisikika mlipuko wa bomu katika jengo la bunge mjini Ankara huku vifaru vikizingira jengo hilo. Aidha wanajeshi waasi walichukua udhibiti wa uwanja wa kimatiafa wa ndege wa katika mji wa Istanbul. Watu zaidi ya 42 wanaripotiwa kuuaawa mjini Ankara na wengine karibu 10 mjini Istanbul kufuatia jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi.

Rais Erdogan amejitokeza mapema Jumamosi asubuhi katika televisheni ya taifa na kusema mapinduzi yamefeli na kwamba waliotekeleza jaribio hilo la mapinduzi ni wahaini na watachukiliwa hatua.

Erdogan amesema jaribio hilo limetekelezwa na kundi la waasi wachache jeshini. Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yildirim ameamuru jeshi kutungua ndege ambazo zimetekwa nyara na wafanya mapinduzi na kuongeza kuwa tayari watu 130 wamekamatwa kufutia jaribio hilo.

Jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi Uturuki limelaaniwa kimataifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amebainisha wasiwasi wake kuhusu jaribio la mapinduzi ya kijeshi Uturuki. Katika ujumbe kupitia twitter Zarif amesema uthabiti na demokrasia ni masuala mawili muhimu kwa watu wa Uturuki. Naye Waziri wa Intelijensia wa Iran Sayyid Mahmoud Alawi amesema Iran inafuatilia kwa karibu matukio ya Uturuki. Amesema vikosi vya kijeshi na maafisa wa usalama Iran wako katika hali ya tahadhari na mipaka ya Iran na Uturuki imedhibitiwa kikamilifu.

 

Tags