Maduro: Uzayuni wa kimataifa unapanga njama za kufanya mapinduzi nchini Venezuela
(last modified Sun, 04 Aug 2024 02:23:16 GMT )
Aug 04, 2024 02:23 UTC
  • Maduro: Uzayuni wa kimataifa unapanga njama za kufanya mapinduzi nchini Venezuela

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema kuwa, Marekani na Uzayuni wa kimataifa wako nyuma ya pazia la kujaribu kufanya mapinduzi nchini Venezuela.

Nicolas Maduro amedokeza kwamba waandamanaji wenye misimamo ya kufurut ada nchini Venezuela wanaungwa mkono kifedha na kisiasa na Uzayuni wa kimataifa, na kusema: Uzayuni pia unaunga mkono njama za mapinduzi Venezuela kupitia ushawishi kwenye mitandao ya kijamii.

Aidha kabla yah apo na katika kikao na waandishi wa habari akiwa katika Kasri ya Miraflores huko Caracas, mji mkuu wa Venezuela, Rais Maduro sambamba na kuonya kuwa serikali yake haitaruhusu kuendelea ghasia na uhalifu nchini humo, amesema hawataruhusu nchi hiyo itumbukie mikononi mwa mabeberu, mafashisti, na wahalifu.

Rais Nicolas Maduro

 

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Venezuela hapo awali ililaani mbinu ya serikali ya Marekani ya "kuongoza mapinduzi" kupitia "uongo na upotoshaji" wa habari ili kuanzisha vurugu na maandamano ya mitaani baada ya uchaguzi wa rais katika nchi hiyo.

Tume ya Uchaguzi ya Venezuela ilitangaza kuwa Maduro ameshinda uchaguzi wa rais wa nchi hiyo kwa kupata 51.2% ya kura, katika uchaguzi wa rais uliofanyika Julai 28. Mkuu wa tume hiyo Elvis Amoroso amesema, Maduro mwenye umri wa miaka 61 amejipatia asilimia 51.2 ya kura, akimshinda mgombea wa upinzani Edmundo González, ambaye alipata asilimia 44.2.

Tags