Aug 11, 2024 06:05 UTC
  • BRICS yakaribisha pendekezo la Iran kwa ajili ya mabadilishano ya fedha

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Russia ameeleza kuwa nchi wanachama wa kundi la BRICs wamekaribisha na kuunga mkono pendekezo la Iran kuhusu kubuni mifumo ya kubadilishana fedha ambayo itazifanya nchi wanachama kutohitajia mifumo ya nchi za Magharibi.

Kundi hilo linaloibukia kiuchumi liliasiwa mwaka 2006 na Brazil, Russia, India na China. Afrika Kusini ilijiunga na kundi hilo mwaka 2010 na baada ya hapo jina la kundi hilo likabadilishwa kutoka BRIC na kuwa BRICS. Kundi la BRICS hivi sasa lina wanachama 9 yaani Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini na pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo pamoja na Misri, Ethiopia, na Imarati zimekuwa wanachama kamili wa kundi la BRICS tangu mwanzoni mwaka huu. 

Nchi waasisi wa kundi la BRICS

Nchi wanachama wa kundi hilo hivi sasa na kiujumla zinaunda karibu asilimia 45 ya jamii yote ya watu duniani na karibu asilimia 30 ya ukubwa wa dunia na wanachama wake wanne yaani Brazil, Russia, India na China zikiwa miongoni mwa nchi 10 za kwanza duniani katika uzalishaji wa pato la taifa kwa mujibu wa usawa wa uwezo wa ununuzi. Aidha ikumbukwe kuwa nchi 9 wanachama wa BRICS, kwa jumla zina zaidi ya asilimia 30 ya pato la taifa kwa kuzingatia usawa wa uwezo wa ununuzi wa nchi zote za ulimwengu, kiwango ambacho kimetajwa kuwa ni kikubwa. 

Nchi hizi zinazoibukia kiuchumi ndani ya kundi hilo zina uwezekano mkubwa wa kuchochea na kuleta matokeo chanya katika uchumi wa dunia, na wakati huo  huo  zinaweza kuratibu na kutekeleza vyema ushirikiano mkubwa wa kiuchumi kati yao. Kwa kuzingatia kuwa moja ya mihimili mitatu mikuu ya BRICS ni masuala ya fedha na uchumi; na zaidi ya hayo, kwa kuzingatia kuwa nchi wanachama wa kundi hilo zinawakilisha sehemu kubwa ya uchumi wa dunia, upo uwezekano wa kutilia maanani upatikanaji wa njia za ufumbuzi na kutekeleza sera za kukabiliana na changamoto za nje khususan vikwazo vya ukandamizaji na kidhalimu vya nchi za Magharibi dhidi ya nchi wanachama. 

Kwa hakika, tunaweza kusema kuwa vikwazo ni tatizo la pamoja linalozikabili baadhi ya wanachama asili wa BRICS. Moja ya sababu kuu za kuongezeka wanachama wa BRICS pia ni kwa ajili ya kufikia mapatano ili kuondokana na changamoto mbalimbali za kiuchumi likiwemo suala la vikwazo. Ni wazi kuwa Marekani inatumia sarafu yake ya dola kama wenzo wa kuziweka chini ya mashinikizo nchi huru duniani. Kuhusiana na suala hilo Kazem Jalali Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Russia ameashiria namna nchi zinazokabiliwa na vikwazo vya  Magharibi na Marekani zinavyoongezeka huku mifumo mingi ya kimataifa ya fedha na benki ikijielekeza upande wa Magharibi na kusema: Nchi wanachama wa kundi la BRICS zinapasa kuzidisha ushirikiano kati yao kwa kuratibu mifumo mipya ya kifedha na kibenki katika mabadilisho mbalimbali ya nchi hizo. Jalali ameongeza kusema: Kuchukua uamuzi kuhusu sarafu ya BRICS kunaweza kuwa na mchango muhimu katika mchakato wa kuachana na matumizi ya dola kwa kuzingatia taathira za wanachama wa BRICS katika uchumi wa dunia. 

Kazem Jalali, Balozi wa Iran nchini Russia 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imejiunga na kuwa mwanachama kamili wa BRICS tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2024 imetoa pendekezo la kuwa na sarafu moja itakayotumiwa na kundi la BRICS jambo ambalo limezingatiwa na kupewa umuhimu pia na wanachama wa kundi hilo. Kazem Jalali ameashiria pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu sarafu ya BRICS ambalo limezingatiwa na Russia ambayo sasa ni mwenyekiti wa kiduru wa kundi hilo na kusema: Mifumo mipya ya kifedha ya kundi la BRICS inaweza kuunganisha wajumbe wa nchi wanachama na hata kutumika katika masuala kama vile kupambana na utakatishaji pesa katika nchi wanachama.