Sep 09, 2024 02:55 UTC
  • Wizi wa simu za rununu waongezeka kwa 150% nchini Uingereza

Uingereza imeshuhudia ongezeko kubwa la viwango vya uhalifu, jambo ambalo sasa linashughulisha sana maoni ya umma. Ongezeko kubwa la visa vya wizi wa mifuko na simu za kisasa za rununu limeifanya serikali ya Uingereza iahidi kuchukua hatua kali dhidi ya uhalifu wa mitaani.

Msururu wa video zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii katika miezi ya hivi karibuni zimeonyesha magenge ya wezi wanaojifunika nyuso zao wakiwa kwenye baiskeli wakiiba simu za rununu za wapita njia katika miji kadhaa ya Uingereza, haswa London, na kuibua hofu katika mitaa ya mji mkuu wa Uingereza. 

Inakadiriwa kuwa takriban watu 78,000 wameibiwa simu au mikoba yao barabarani mwaka huu wa 2024, ikiwa na maana ya zaidi ya matukio 200 ya wizi wa mitaani kwa siku. Idadi hii ni zaidi ya mara mbili ya matukio yaliyorekodiwa katika kipindi kama hicho hadi Machi 2023, ambapo matukio 31,000 ya wizi wa simu za kiganjani yalirekodiwa nchini Uingereza.

Utafiti mpya uliofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza kuhusu suala hili umefichua kwamba, makadirio ya data za uchunguzi wa uhalifu kwa miezi 12 iliyopita yanaonyesha kwamba zaidi visa 200 vya wizi vinarikodiwa kila siku katika mitaa ya Uingereza na Wales, kiwango ambacho ni cha juu zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 ya karibuni.

Makadirio yaliyochapishwa kutokana na Utafiti wa Uhalifu kwa Uingereza na Wales pia yameonyesha kuwa zaidi ya theluthi moja ya uhalifu wa wizi (36%) ulihusisha wizi wa simu za rununu katika mwaka uliopita.