Sep 13, 2024 07:35 UTC
  • Baraza la Usalama la UN
    Baraza la Usalama la UN

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejadili athari za mashambulizi mawili ya anga yaliyofanywa Israel juzi Jumatano kwenye shule inayowahifadhi waliokimbia wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, ambayo yameua raia 18, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi wengine wengi.

Mashambulizi hayo ya Israel pia yameua wafanyakazi sita wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Algeria, ambayo ndiyo iliyotoa wito wa kuitishwa kikao hicho cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, imelaani vikali mashambulizi hayo na kueleza wasiwasi wake mkubwa kutokana na shule kuwa shabaha kuu za jeshi la Israel, na kuuliwa raia wengi wasio na hatia. Algeria imesema hilo ni shambulio la tano kufanywa na Israel dhidi ya shule  ya Al-Jaouni inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Algeria imesisitiza kuwa, miundombinu na wafanyakazi wa masuala ya kibinadamu wana kinga maalumu chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, na kwamba kushambulia vitu hivyo ni uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa.

Algeria imekiambia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, jeshi la utawala ghasibu wa Israel limeshambulia kwa makusudi wafanyakazi wa huduma za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la UNRWA, ambalo tayari imepoteza zaidi ya wafanyakazi 220 waliouawa na jeshi la Israel.

Wajumbe wa Baraza la Usalama waliotoa hotuba katika kikao hicho wamesisitiza kwamba hali hiyo hatari unahitaji hatua za haraka za Baraza la Usalama. Hata hivyo kwa mara nyingine tena, Marekani imeukingia kifua utawala katili wa Israel kwa kuzuia baraza hilo kuchukua hatua yoyote dhidi ya mauaji hayo. 

Akizungumzia shambulio hilo katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii wa X, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema: "kinachotokea Gaza hakikubaliki hata kidogo. Shukle iliyogeuzwa makazi ya takribani watu 12,000 imeshambuliwa tena na Israel" na akaongeza kwa kusema: "wenzetu sita wa UNRWA ni miongoni mwa waliouawa".