Sep 18, 2024 07:55 UTC
  • Kampuni ya Taiwan yakanusha kutengeneza vifaa vya mawasiliano vilivyoripuka Lebanon

Kampuni ya Gold Apollo ya Taiwan imekanusha kuwa ndiyo iliyotengeneza vifaa vya mawasiliano vya 'Pagers' vilivyoripuka nchini Lebanon.

Katika taarifa iliyotoa mapema leo, kampuni hiyo ya Apollo Gold Corporation imesema, imetoa idhini ya muda mrefu ya kutumiwa lebo ya binafsi na ushirikiano wa wakala wa kikanda na kampuni ya Ulaya ya BAC, ambayo ina leseni ya kutumia chapa yake. 
Taarifa hiyo imefafanua kuwa kulingana na makubaliano hayo, Apollo Gold Corporation imetoa idhini kwa kampuni ya BAC kutumia chapa ya biashara yake kwa mauzo ya bidhaa katika maeneo maalumu, lakini muundo na utengenezaji wa bidhaa unashughulikiwa kikamilifu na BAC.
Mossad

"Kuhusu ripoti za karibuni za vyombo vya habari kuhusu pager ya AR-924, tunafafanua kuwa muundo huu unatengenezwa na kuuzwa na BAC. Tunatoa tu idhini ya chapa ya biashara na hatuhusiki katika muundo au utengenezaji wa bidhaa hii," imebainisha taarifa hiyo.

 
Mapema, mwanzilishi wa kampuni hiyo Hsu Ching-kuang naye pia alikanusha kuhusika kampuni yake katika utengenezaji wa vifaa hivyo.
 
Kulingana na kituo cha habari cha Sky News Arabia, Shirika la ujasusi la Israel Mossad lilitega viripuzi kwenye betri za vifaa vya 'pager' vilivyoripuka jana Jumanne nchini Lebanon, na kuua watu tisa na kujeruhi karibu wengine 2,750, wakiwemo 200 ambao hali zao ni mahututi.
 
Gazeti la New York Times, likiwanukuu maafisa waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina, limesema vifaa vya  mawasiliano vya 'Pagers' ambavyo Hizbullah ya Lebanon iliviagiza kutoka kampuni ya Gold Apollo ya Taiwan 'vilitiwa mkono' kabla ya kuwasili nchini humo.../

 

Tags