Baqaei: Kampeni ya kueneza uongo dhidi ya Iran imefichuliwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135966-baqaei_kampeni_ya_kueneza_uongo_dhidi_ya_iran_imefichuliwa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran mapema leo ameandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X, akionyesha video iliyorushwa hewani na Channel 12 ya Israel ambapo mwanamke Muisraeli anashangazwa na tangazo la picha yake akitajwa kuwa ni miongoni mwa "waliouawa" katika maandamano nchini Iran.
(last modified 2026-01-27T10:07:37+00:00 )
Jan 27, 2026 10:07 UTC
  • Esmail Baqaei
    Esmail Baqaei

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran mapema leo ameandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X, akionyesha video iliyorushwa hewani na Channel 12 ya Israel ambapo mwanamke Muisraeli anashangazwa na tangazo la picha yake akitajwa kuwa ni miongoni mwa "waliouawa" katika maandamano nchini Iran.

Baqaei ameandika: "Mwanamke anayeitwa Noya Zion - kwa mujibu wa madai ya Channel 12 ya Israel - "aliuawa" wakati wa maandamano nchini Iran - na mtandao huo hata ulionyesha picha yake kama ushahidi."

Esmail Baqaei ameendelea kuandika: "Mwanamkke huyo, ambaye ameshtuka, amerusha video inayoonyesha kwamba yuko nyumbani kwake na yuko salama kabisa, na hajawahi kusafiri kwenda Iran."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa: "Jambo hili peke yake linazungumzia mengi kuhusu kampeni ya kimfumo ya kueneza uongo mkubwa kama wa Hitler na kutangaza taarifa za uongo na masimulizi bandia dhidi ya taifa la Iran."

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, kiijana wa kike wa kiisraeli aitwaye Noya Zion ameshtuka baada ya kuona picha yake inaonyeshwa kwenye televisheni ya taifa ya Israel kama mmoja wa watu waliouawa katika maandamano nchini Iran, mkasa ambao umezidi kudhihirisha jinsi utawala huo wa kizayuni unavyosambaza habari feki na za uwongo kuhusu machafuko ya hivi karibuni nchini Iran na namna serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ilivyokabiliana nayo.

Zion, ambaye hajawahi kutia mguu wake katika ardhi ya Iran, alikuwa nyumbani kwao jana Jumatatu alipotazama Chaneli ya 12 ya habari ya Israel na kuona picha yake ikionyeshwa chini ya kichwa cha habari kilichodai "Wayahudi Wanne Wauawa Katika Maandamano nchini Iran."

Ripoti hiyo ilimtambulisha Zion kiuwongo kama Sanaz Javaherian, mtu ambaye chaneli hiyo imedai alikuwa mwandamanaji aliyekamatwa na kupigwa hadi kufa na askari usalama wa Iran.

"Sikuwahi katu kufikiria kama lingenitokea hili maishani mwangu... Niko nyumbani kwetu!" alisema Zion katika video aliyoisambaza haraka kwenye mitandao ya kijamii, akijirekodi pamoja na matangazo ya upotoshaji yaliyorushwa hewani na televisheni ya utawala wa kizayuni.

Noya Zion

Kipande hicho cha video kimezidi kudhihirisha upuuzi wa habari bandia na za upotoshaji zinazosambazwa na utawala wa kizayuni wa Israel na washirika wake wa Kimagharibi kuhusu hali ya mambo nchini Iran.