Erdogan: Marekani haitaki Ukraine iwe mwanachama wa NATO
Rais wa Uturuki amesema kuwa, ingawaje Marekani ndiye mpinzani mkuu wa Ukraine kujiunga na Shirika la la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), lakini pia nchi nyingi za jumuiya hiyo zinapinga Kyev kupewa uanachama.
Huku 'mpango wa ushindi' wa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ukisisitiza haja ya nchi yake kujiunga na NATO, lakini Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameiambia NBC News kwamba: "Marekani, kwanza kabisa, haitaki kuona Ukraine inakuwa mwanachama wa NATO. Na nchi nyingi za NATO pia hazitaki Ukraine kuwa nchi mwanachama."
Alipoulizwa moja kwa moja iwapo Ankara itakubali Ukraine kujiunga na NATO, Erdogan alijibu kwamba, "Tutafuata wimbi la matukio, kufanya mashauriano, na kufikia uamuzi wa mwisho unaofaa. Haya si maamuzi ya kuharakishwa na kufanyiwa pupa.”
Juni mwaka huu pia, Sergey Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisema ni jambo lisiloyumkinika kwa Ukraine kuwa mwanachama wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO. Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg alisema hivi karibuni kuwa, ili Ukraine ikubaliwe kujiunga na muungano huo wa kijeshi wa Magharibi, sharti ishinde vita dhidi ya Shirikisho la Russia.
Baadhi ya nchi za Magharibi zinataka kutumwa askari wa NATO nchini Ukraine, lakini zingine zinasisitiza kuwa haziungi mkono mpango huo zikionya kuwa, hatua hiyo inaweza kuzusha Vita vya Tatu vya Dunia.
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amekuwa akiwashinikiza viongozi wa Magharibi waipe Kyev silaha na vifaa zaidi vya kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Moscow.