Jenerali Vahidi: Vitisho vya Maadui vinatokana na woga na hofu yao
Naibu kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, amesisitizia wajibu wa kuendelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuunga mkono Mhimili wa Muqawama na kusema kuwa: "Vitisho na bwabwaja za maadui zinatolewa kutokana na woga na hofu waliyo nayo na hazitaathiri njia ya Jamhuri ya Kiislamu na ya Kambi ya Muqawama."
Mwandishi wa shirika la habari wa Mehr amemnukuu, Jenerali Ahmad Vahidi, naibu kamanda wa jeshi la SEPAH akisema hayo pambizoni mwa kumbukumbu za kuadhimisha miaka sita ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Hajj Qasem Soleimani, aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, zilizofanyika jana Alkhamisi katika Msikiti wa Imam Khomeini (MA) hapa Tehran, na kusema: "Kwa taufiki na baraka za Mwenyezi Mungu, Mhimili wa Muqawama uko kwenye njia yake ya kuzidi kustawi na kuwa imara na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono ukuaji, maendeleo na ustawi huo kwa nguvu zake zote."
Ameongeza kuwa: "Njia na chuo cha shahid Luteni Jenerali Hajj Qassem Soleimani haitaachwa kamwe, na tunaendelea na njia na maadili ya shahidi huyu mkubwa kwa nguvu zetu zote."
Akijibu vitisho vya hivi karibuni vya maadui, Naibu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema: "Kauli kama hizo ni maneno ya hofu yanayotolewa watu wenye woga mkubwa kwa sababu maadui wameshindwa kukabiliana na kambi ya Muqawama. Hayo ni maneno ya watu waliokata tamaa mbele ya nguvu zisizozuilika za Kambi ya Muqawama."
Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, aliuawa shahidi Januari 3, 2020 katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq ya al Hashd al Sha'abi na wanamapambano wengine wanane, wakati alipoelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.