Karibu dola bilioni 50, deni la taifa la Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135020-karibu_dola_bilioni_50_deni_la_taifa_la_libya
Deni la taifa la Libya lilikuwa ni karibu dola bilioni 50 za Marekani mwaka 2024, hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya Ofisi ya Ukaguzi ya Libya, ambayo huwa inatolewa mwishoni mwa kila mwaka unaofuata.
(last modified 2026-01-02T06:53:55+00:00 )
Jan 02, 2026 06:53 UTC
  •  Karibu dola bilioni 50, deni la taifa la Libya

Deni la taifa la Libya lilikuwa ni karibu dola bilioni 50 za Marekani mwaka 2024, hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya Ofisi ya Ukaguzi ya Libya, ambayo huwa inatolewa mwishoni mwa kila mwaka unaofuata.

Kwa mujibu wa ofisi hiyo ya ukaguzi, jumla ya deni la taifa la Libya ilifikia dinari bilioni 270 za Libya (karibu dola bilioni 49.8), ikiwa ni pamoja na dinari bilioni 84 inazodai Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) yenye makao yake makuu Tripoli na dinari bilioni 186 unazodai utawala wa mashariki ulioteuliwa na Baraza la Wawakilishi la Libya.

Ripoti ya Jumatano ya Ofisi hiyo ya Ukaguzi ilisema kuwa, viwango vya deni vimebaki bila ya kubadilika kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 2020.

Takwimu za deni hilo zinakaribia kufanana na pato la kiuchumi la Libya, huku takwimu za Benki ya Dunia zikionesha kuwa pato la taifa la Libya mwaka 2024 lilikuwa ni dola bilioni 46.6.

Libya imekumbwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa kwa muda mrefu tangu NATO ilipoivamia kijeshi nchi hiyo mwaka 2011 kwa madai ya kuunga mkono wananchi na kumuondoa madarakani Muammar Gaddafi.

Mpaka hivi sasa Libya haijawa na utulivu wa kuaminika wa kisiasa na hivi sasa inaongozwa na serikali mbili na mabunge mawili. Moja ni Serikali ya Umoja wa kitaifa GNU, inayoongozwa na Abdul Hamid Dbeibah upande wa magharibi inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, na nyingine ni serikali ya mashariki inayoongozwa na Osama Hammad na inayoungwa mkono na Bunge.