Gazeti la Marekani lathibitisha makombora ya Iran yaliharibu vituo vya kijeshi vya 'Israel'
Gazeti la Washington Post limethibitisha kuwa vituo kadhaa vya kijeshi na vya "usalama" vya utawala wa Israel viliharibiwa vibaya na makombora yaliyorushwa na Iran wakati wa operesheni ya kulipiza kisasi hivi karibuni.
Likiripoti siku ya Ijumaa, gazeti hilo la kila siku limesema kwamba picha na taswira zinaonyesha kuwa makombora zaidi ya 24 yamelenga na kuharibu kwa uchache maeneo matatu muhimu ya kijeshi na kijasusi ya utawala huo.
Gazeti hilo limethibitisha kuwa makombora zaidi ya 24 yalilenga Uwanja wa Ndege wa Jeshi la Anga wa Nevatim, kusini mwa jangwa la Negev, na makombora mengine matatu yalitua katika kambi ya kijeshi ya Tel Nof katikati mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Hali kadhalika gazeti la Washington Post limeandika kuwa makombora yasiyopungua mawili pia yalitua karibu na makao makuu ya shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni, Mossad huko Tel Aviv.
Ripoti hiyo imesema: "Wachambuzi wameiambia Washington Post kuwa picha zilizochunguzwa zinaonyesha kuwa makombora yalilenga maeneo hayo moja kwa moja na wala si mabaki ya makombora yaliyotunguliwa."
Gazeti hilo limeandika kuwa yamkini makombora ya Iran yalisababisha uharibufu mkubwa zaidi ya inavyoripotiwa.
Utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani, hata hivyo, zimedai kwamba makombora hayo yamesababisha "uharibifu mdogo " huku jeshi la Israel pia likidai kuwa kambi zake za kijeshi na kijasusi "zinafanya kazi kama kawaida."
Ripoti hiyo imekuja baada ya Jamhuri ya Kiislamu kurusha mamia ya makombora kuelekea vituo vya kijeshi na kijasusi vya utawala haramu Israel katika Operesheni ya Ahadi ya Kweli II siku ya Jumanne ili kulipiza kisasi kuuawa shahidi mkuu wa Hamas Ismail Haniya, kiongozi wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah na kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC Abbas Nilforoushan.
Kwa mujibu wa IRGC, asilimia 90 ya makombora yalilenga shabaha zilizokusudiwa, na kukwepa mifumo ya makombora ya utawala huo ambao umekuwa ukijigamba kuwa una uwezo mkubwa wa kijeshi.