Erdogan: Iwe ni karibuni au baadaye, Israel italipa kwa mauaji ya kimbari inayoendeleza Ghaza
(last modified Wed, 09 Oct 2024 02:29:16 GMT )
Oct 09, 2024 02:29 UTC

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema, iwe iwavyo utawala wa Kizayuni wa Israel utalipa kwa mauaji ya kimbari ambayo umekuwa ukiendelea kuyafanya katika Ukanda wa Ghaza kwa mwaka mmoja sasa.

Katika ujumbe alioweka kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X, Erdogan amesema: "isisahaulike kuwa iwe ni karibuni au baadaye, Israel italipa kwa mauaji haya ya kimbari ambayo yamekuwa yakiendelea kwa mwaka sasa".
 
Mbali na kusisitizia haja ya kuchukuliwa hatua za pamoja dhidi ya Israel, Rais wa Uturuki amesema: "kama vile ambavyo muungano wa pamoja wa ubinadamu ulimsimamisha Hitler, Netanyahu na mtandao wake wa mauaji nao pia watasimamishwa kwa njia hiyo hiyo."
 
Erdogan amebainisha pia kwamba, wanaokufa siku hizi huko Ghaza, Palestina na Lebanon si wanawake, watoto wadogo, vichanga na raia wasio na hatia tu, bali unakufa pia ubinadamu na mfumo wa kimataifa.
Kutoka kushoto: Erdogan, Hitler, Netanyahu

Rais wa Uturuki ametuma salamu za rambirambi pia kwa watu wa Palestina na Lebanon kutokana na mauaji ya makumi ya maelfu ya watu yaliyofanywa na utawala haramu wa Israel tangu tarehe 7 Oktoba, 2023.

Utawala ghasibu wa Kizayuni ungali unaendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza, kufuatia Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa na Wanamuqawama wa Hamas Oktoba mwaka jana, licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusimamishwa mara moja vita hivyo.

Tangu wakati huo hadi sasa, karibu Wapalestina 42,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameshauawa shahidi, na zaidi ya wengine 97,100 wamejeruhiwa.../

Tags