Jumanne, Aprili 22, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 23 Mfunguo Mosi Shawwal 1446 Hijria sawa na tarehe 22 Aprili 2025 Milaadia.
Katika siku kama ya leo miaka 334 iliyopita alifariki dunia Sayyid Neematulllah Jazairi aliyekuwa faqihi na mpokezi mkubwa wa Hadithi wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 62.
Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, Hadithi, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu na alistahamili mashaka mengi katika njia ya kulingania sheria za dini ya Kiislamu.
Sayyid Neematullah Jazairi ameandika vitabu kadhaa vya thamani kama Madinatul Hadith, Qiswasul Anbiyaa na Hidayatul Muuminin.

Siku kama ya leo miaka 301 iliyopita, alizaliwa Immanuel Kant, mwanafalsafa mkubwa wa Ujerumani katika eneo la Königsberg.
Baada ya kuhitimu masomo katika taaluma ya hisabati, theolojia na falsafa Kant alijishughulisha na kazi ya ufundishaji vijijini. Baadaye msomi huyo alifanikiwa kuwa mhadhiri wa falsafa katika chuo kikuu cha mji alikozaliwa wa Königsberg.
Katika miaka yote ya utafiti wake na kufundisha falsafa, alipata kuandika vitabu tofauti ambavyo baadhi vipo katika maktaba kubwa duniani. Kadhalika mwanafalsafa huyo mkubwa alifanikiwa kuasisi mfumo wa kifikra maalumu katika uga huo.
Kwa imani ya Immanuel Kant, ndani ya mwanadamu kuna hisia maalumu ya kitabia ambayo huweza kutoa hukumu kwamba kitendo hiki ni chema na kile ni kiovu. Hii ikiwa na maana kwamba, mwanadamu binafasi anaweza kutenda mema na maovu, lakini ile hisia yake ya kitabia ndio huweza kumueleza kwamba kitendo fulani ni chema au kibaya na kwamba lau kama si kuwepo kwa hisia hiyo, basi mwanadamu asingeweza mwenyewe kujilaumu baada ya kutenda jambo fulani.
Immanuel Kant alifariki dunia tarehe 12 Februari 1904 mjini Königsberg akiwa na umri wa miaka 80 na aliishi maisha yake yote akiwa kapera.

Siku kama hii ya leo miaka 130 iliyopita wananchi wa Cuba kwa mara nyingine tena walianzisha mapambano ya kupigania uhuru wao kutoka kwa wakoloni wa Uhispania.
Hayo yalikuwa mapambano yao ya tatu katika nusu ya pili ya karne ya 19 Miladia kwa ajili ya kutaka kujitawala. Uhispania ilituma wanajeshi laki tatu nchini humo kwa ajili ya kupambana na wanamapinduzi hao. Kufuatia vurugu hizo Marekani ilitumia fursa hiyo na kwa kisingizio cha kulipuliwa meli yake ya kivita karibu na pwani ya Cuba mwaka 1898 Miladia, kuingia katika vita hivyo dhidi ya Uhispania.
Manuwari za kivita za Uhispania ziliangamizwa katika maji ya Cuba na hatimaye nchi hiyo ya Amerika ya Latini ikakaliwa kwa mabavu na Marekani. ****
Miaka 121 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani, Robert Oppenheimer.
Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia.
Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani.

Miaka 77 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, yaani tarehe 22 Aprili 1948, Wazayuni waliushambulia mji wa bandari wa Haifa huko kaskazini magharibi mwa Palestina wakati wa kukaribia kuanzishwa utawala haramu wa Israel.
Wazayuni waliwauwa shahidi Wapalestina 500 katika mashambulizi hayo makubwa na kuwajeruhi wengine 200 ambao walikuwa wanawake na watoto waliokimbilia huko Haifa wakisubiri kupelekwa katika maeneo mengine.

Miaka 64 iliyopita siku hii, Aprili 22, 1961, jaribio la Jeshi la Siri la Ufaransa la kufanya mapinduzi nchini Algeria lilisababisha vifo vya watu wasiopungua 1,200 katika mji mkuu wa nchi hiyo, Algiers.
Baada ya Jenerali de Gaulle kuingia madarakani nchini Ufaransa, alizungumzia haki ya watu wa Algeria kuamua hatima yao wenyewe. Hata hivyo alitarajia kuweka madarakani kundi lake la mawakala nchini Algeria.
Wakati huo huo, wanajeshi waliokuwa na misimamo mikali wa Wafaransa waliunda kundi lililoitwa Shirika la Jeshi la Siri, na ajenda yao ilikuwa kujenga hofu katika nyoyo za watu wa Algeria na pia Wafaransa wahafidhina.
Hatua za jeshi la siri la Ufaransa, lililotaka kuendeleza utawala serikali ya Paris huko Algeria, zilisababisha uasi Aprili 22, 1961, na hatimaye kuuawa Waalgeria 1,200.
Watu wa Algeria walipata uhuru mwaka 1962 baada ya Ufaransa kuua Waalgeria karibu milioni moja na kuikoloni nchi hiyo kwa miaka 130.

Na siku kama ya leo miaka 46 iliyopita Imam Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuundwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH).
Kwa mujibu wa amri hiyo, jukumu kuu la jeshi hilo ni kulinda Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya maadui wa ndani na nje. Baada ya kuundwa, jeshi la SEPAH lilikabiliana na makundi yaliyopinga Mapinduzi ya Kiislamu, yaliyoanzisha mapambano ya silaha katika pembe mbalimbali za Iran na kuweza kuzima njama za maadui.
Aidha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi liliweza kudhihirisha uwezo mkubwa wakati wa vita vya kulazimishwa kati ya Iraq na Iran vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta Saddam Hussein kwa lengo la kuyaangamiza Mapinduzi ya Kiislamu na kuigawa Iran.
