Zambia yaripoti visa 20 vipya vya kipindupindu ndani ya saa 24
Zambia imeripoti visa 20 vipya vya kipindupindu katika kipindi cha saa 24 zilizopita hadi Jumatatu, huku mji mkuu Lusaka ukichangia visa 11 kati ya hivyo.
Hayo yamedokezwa Jumatatu na Waziri wa Afya, Elijah Muchima ambaye ameongeza kuwa visa vinne kati ya vilivyobaki viliripotiwa katika mji wa Nakonde, uliopo mpakani na Tanzania, visa vitatu katika eneo la Choma mkoa wa Kusini, na visa viwili katika Mpulungu, mji ulioko katika fukwe za Ziwa Tanganyika.
Muchima amewaeleza waandishi wa habari kwamba hakuna vifo vilivyoripotiwa kutokana na visa hivyo vipya, na kwa sasa idadi ya wilaya zilizo na maambukizi hai ya kipindupindu imefikia saba.
Ameongeza kuwa: “Lusaka bado ndicho kichocheo kikuu cha mlipuko huu, ikiwa na maambukizi yaliyoenea kwa kiwango cha chini lakini katika vitongoji vingi, huku Mpulungu ikiendelea kushuhudia wimbi la pili la maambukiz."
Muchima pia amesema kuwa mvua kubwa zilizonyesha kwa wingi katika baadhi ya maeneo ya nchi zimesababisha mafuriko, hali inayoongeza hatari ya magonjwa yanayosambazwa kupitia maji.
Amewahimiza wananchi kuzingatia usafi wa mazingira, kutafuta matibabu mapema, na kufuata miongozo ya afya ya umma iliyotolewa na serikali.