Nicaragua yakata uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel
Serikali Nicaragua imetangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na Israel kuendelea na mauaji ya kimbari huko Gaza.
Serikali ya Nicaragua imewalaani viongozi wa Israel na kuwataja kuwa 'mafashisti' kutokana na kutenda 'mauaji ya halaiki' katika vita vyao dhidi ya Gaza.
Nicaragua imetangaza kwamba itavunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel, na hivyo kuongezeka kutengwa Israel kimataifa wakati wa vita vyake huko Gaza.
Rosario Murillo Makamu wa Rais wa Nicaragua ametangaza hatua hiyo kwa vyombo vya habari vya serikali baada ya Bunge la Congress la nchi hiyo kupitisha azimio la kutaka kuchukuliwa hatua baada ya kuadhimisha mwaka mmoja wa hujuma na mashambulio ya kinyama ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Katika miaka ya hivi karibuni Israel imeendelea kutengwa kimataifa kutokana na jinai na mauajii yake ya kimbari huko Palestina ambapo kila leo idadi ya mataifa yanayokata uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo ghasibu inazidi kuongezeka.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, mwezi Mei mwaka huu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) hatimaye liliipigia kura ya ndio rasimu ya uanachama kamili wa Palestina katika umoja huo baada ya Marekani kukwamisha suala hilo kwa miaka kadhaa.
Rasimu ya azimio la kuunga mkono uanachama kamili wa Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambayo ilipasishwa kwa kura 143 za ndio, 9 za hapana na nchi 25 zikijizuia kupiga kura inaipatia Palestina haki na mafao zaidi katika Umoja wa Mataifa.