Indonesia yayatolea wito mataifa ya Asia Mashariki kuitambua nchi ya Palestina
Indonesia imetoa wito kwa mataifa ya Asia Mashariki kuitambua nchi ya Palestina na kuitaka jamii ya kimataifa isimamie sheria za kimataifa na ubinadamu.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Ma'ruf Amin alipozungumza katika mkutano wa kilele wa Asia Mashariki mjini Vientiane, Laos, na kutahadharisha kuwa bila kuchukuliwa hatua kuhusiana na kadhia ya Palestina migogoro mingi mipya inaweza kuibuka.
"Kama viongozi, lazima tuchukue msimamo wa kusimamia sheria za kimataifa na ubinadamu. Msiwe mnachagua katika kutekeleza sheria za kimataifa. Hili likiendelea, nina hofu kwamba migogoro mingi mipya itaibuka," amesisitiza Amin na kuongezea kwa kusema:"(kwa hiyo), naomba nchi ambazo hazijaitambua Palestina zifanye hivyo mara moja".
Makamu wa Rais wa Indonesia ametilia mkazo sheria za kimataifa kuheshimiwa na kila mtu bila ubaguzi.
Idadi ya nchi zilizoitambua Palestina hadi sasa imefikia 146 kufuatia maamuzi ya Uhispania, Norway, Ireland, Slovenia, Armenia, Bahamas, Trinidad na Tobago, Jamaica na Barbados ya kuitambua nchi hiyo.
Inafaa kuashiria kuwa, utawala wa Kizayuni Israel ungali unaendeleza mashambulizi ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Ghaza ulivyoanzisha Oktoba mwaka jana tangu harakati ya Muqawama ya Palestina ya Hamas ilipotekeleza operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa, licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotaka kusimamishwa vita mara.
Zaidi ya Wapalestina 42,000 wameuawa shahidi, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na karibu 97,900 wamejeruhiwa.../