Kikao cha Moscow na suala la wahamiaji wa Afghanistan
(last modified Mon, 14 Oct 2024 02:24:35 GMT )
Oct 14, 2024 02:24 UTC
  • Kikao cha Moscow na suala la wahamiaji wa Afghanistan

Mjumbe Maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Afghanistan amesema kuwa kikao kilichofanywa hivi karibuni na nchi jirani za Afghanistan huko Moscow, kilifanyika katika fremu ya mpango wa kikanda wa kuisaidia Afghanistan katika kupambana na ugaidi na kuisaidia kupata maendeleo, ili kuepusha wimbi la wahamiaji kutoka nchi hiyo.

Akifafanua suala hilo, Hassan Kazemi Qomi, Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Afghanistan ameashiria duru ya sita ya kikao hicho huko Moscow, mji mkuu wa Russia  na kusisitiza kuwa licha ya migogoro ya Palestina na Lebanon, lakini suala la Afghanistan bado ni suala muhimu linalozingatiwa kieneo.

Miongoni mwa changamoto na matatizo yanayozikabili nchi jirani na Afghanistan ni kuwa nchi hiyo ni kitovu muhimu cha harakati za makundi ya kigaidi yanayoendelea kuenea katika eneo na ongezeko la magendo ya dawa za kulevya na wahajiri.

Wakimbizi wa Afghanistan

Nchi za kanda hiyo, haswa katika miaka mitatu 3 iliyopita ambapo Afghanistan imepitia mabadiliko muhimu ya kisiasa, zimekabiliwa na hali ngumu sana ya wahamiaji kutoka nchi hii kuliko wakati mwingine wowote, jambo ambalo limezisababishia matatizo mengi ya kijamii na kiusalama. Hivyo, nchi za eneo na hasa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita zimekuwa zikitekeleza mikakati ya kuwapanga upya wahamiaji wa Afghanistan. Kuhusu suala hilo, vikao ambavyo vimekuwa vikifanywa na nchi jirani katika fremu ya Mfumo wa Moscow vimechukua uamuzi muhimu wa kuandaa mazingira yanayofaa ya kuhusu maendeleo huko Afghanistan, uamuzi ambao bila shaka unaweza kuwa na nafasi muhimu katika kupunguza wimbi la wahajiri na kutatua matatizo na changamoto nyingine nyingi zinazoikabili nchi hiyo.

Kwa maelezo hayo, mojawapo ya njia za kutatua matatizo ya Afghanistan na kuwasaidia watu wa nchi hii ni kutumiwa uwezo wa kikanda na wa nchi jirani. Pamoja na kuwa ni nchi za Magharibi, haswa Marekani, ndizo zimesababisha matatizo yote haya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa huko Afghanistan, lakini nchi hizo zimepuuza kabisa matatizo hayo, na sasa ni nchi  jirani ndizo kwa namna moja au nyingine zinapasa kubuni mipango ya kikanda kwa lengo la kukabiliana na changamoto za Afghanistan na kuisaidia kimaendeleo ili kuzuia mafuriko zaidi ya wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi hiyo.

Tunakumbusha kuwa mkutano wa sita wa "Moscow Format" kuhusu Afghanistan uliofanyika Ijumaa iliyopita huko Moscow katika ngazi ya wajumbe maalumu na maafisa wa ngazi za juu kutoka serikali za Taliban, China, India, Iran, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Pakistan, Russia, Tajikistan na Uzbekistan. Hii ni katika hali ambayo suala la Afghanistan ni suala lililosahaulika kabisa kwa nchi za Magharibi.