Maduro: Benjamin Netanyahu ni zimwi lililotengenezwa na Marekani
Mapema leo asubuhi Rais wa Venezuela amemshambulia vikali waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu kutokana na jinai za kuchupa mipaka anazofanya nduli huyo wa Ghaza na Lebanon.
Vyombo vya habari vimemnukuu Rais Nicolas Maduro wa Venezuela akisema kuwa, Benjamin Netanyahu ni zimwi lililotengenezwa na Marekani kiasi kwamba hata Hitler wa Ujerumani hakuwa na uthubutu wa kutenda jinai zinazofanywa na Netanyahu hivi sasa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Maduro amesema kuwa, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa dola pandikizi la kigaidi la Israel ni nduli na zimwi lililotengenezwa na madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.
Rais huyo wa Venezuela amegusia jinai za Wazayuni katika eneo hili la Asia Magharibi na kuongeza kuwa, Netanyahu hivi sasa anafanya mauaji ya kizazi huko Palestina na Lebanon na kwamba kinachoshuhudiwa hivi sasa si vita bali ni mauaji ya umati yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wasio na hatia.
Kwa upande wake televisheni ya Al Mayadeen nayo imemnukuu Rais huyo wa Venezuela akisema kuwa, mpaka hivi sasa Netanyahu ana kiburi cha kutoa amri dhidi ya hata Umoja wa Mataifa bali amefikia hata kushambulia askari wa umoja huo huko Lebanon bila ya kuchukuliwa hatua zozote za kinidhamu.
Rais Maduro ameongeza kuwa, hata Hitler hakuwa na uthubutu wa kufanya jinai zinazofanywa na zimwi hili (Netanyahu) lililotengenezwa na nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani.