Medvedev: Russia itatumia silaha za nyuklia ikiwa uwepo wake utatishiwa
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Shirikisho la Russia, Dmitry Medvedev amesema kuwa Marekani inafanya makosa ikiwa inaamini kwamba Moscow haitatumia silaha za nyuklia iwapo uwepo wake utatishiwa.
Katika taarifa yake ya jana Jumamosi kwa idhaa ya RT ya Russia, Medvedev aliitaka Washington kushughulikia kwa uzito tishio la Moscow la kutumia silaha za nyuklia, akisema kuwa hilo litaepusha kuzuka kwa Vita vya Tatu vya Dunia.
Medvedev, ambaye aliwahi kuwa rais wa Russia, amesema: "Maafisa wakuu nchini Merekani hawataki kutokea vita vya tatu vya dunia, lakini kwa sababu fulani wanaamini kwamba, Warusi hawatavuka mstari fulani, lakini wanakosea."
Ameongeza kuwa, Moscow inaamini kwamba taasisi za sasa za Marekani na Ulaya hazina hekima na dira ya mwanadiplomasia mwendazake wa Marekani, Henry Kissinger.
Dmitry Medvedev, amesema: "Tunapozungumzia uwepo wa nchi yetu, kama rais wetu anavyosema mara kwa mara, hatutakuwa na chaguo lingine, isipokuwa kutumia silaha za nyuklia."
Matamshi hayo yametolewa sambamba na kusonga mbele kwa vikosi vya jeshi la Russia mashariki mwa Ukraine, na Magharibi ikiendelea kutoa silaha na fedha kwa serikali ya Kiev.
Kwa upande wao, wanadiplomasia wa Marekani wanakiri kwamba uhusiano kati ya Washington na Moscow unapitia kipindi kibaya zaidi tangu enzi za Vita Baridi.