Sababu za Chad kusimamisha utoaji visa kwa raia wa Marekani
(last modified Sat, 07 Jun 2025 13:25:50 GMT )
Jun 07, 2025 13:25 UTC
  • Sababu za Chad kusimamisha utoaji visa kwa raia wa Marekani

Kufuatia uamuzi wa Rais wa Marekani wa kuwawekea vikwazo vya usafiri raia wa nchi 12 ambazo kimsingi ni za Waislamu na za Kiafrika, nchi nyingi kati ya hizo zimeuchukulia uamuzi huo kuwa unatokana na siasa za utaifa na zinaziponga uhamiaji za Rais Donald Trump.

Mbali na Iran, ambayo imeutaja uamuzi huo kuwa wa kibaguzi, ulio kinyume cha sheria, ishara ya kuendelea kwa siasa za chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi wa rangi, na kutangaza kwamba hatua hizo, badala ya kupambana na ugaidi, zinachochea kutoaminiana kati ya mataifa, migawanyiko na mivutano ya kimataifa, Chad pia imelaani hatua hiyo na kusimamisha kwa muda utoaji wa visa kwa raia wa Marekani. Rais wa Chad amesema nchi hiyo imechukua hatua hiyo kwa ajili ya kutetea heshima na fahari yake ya kitaifa.

Amri hiyo ya Trump, ambayo imepangwa kutekelezwa Juni 9, ni mwendelezo wa sera zile zile zilizopitishwa huko nyuma na serikali ya Trump dhidi ya nchi kadhaa zenye wakaazi wengi wa Kiislamu. Katika agizo hilo, serikali ya Marekani imetaja sababu kuu ya kuweka vikwazo vya usafiri dhidi ya raia wa nchi hizo kuwa ni kulinda usalama wa taifa dhidi ya vitisho vya kigaidi, kwa madai kuwa baadhi ya nchi hazikidhi viwango vinavyohitajika katika masuala ya upashanaji taarifa za usalama au pasi za kielektroniki. Chad, Somalia, Libya, Yemen, Syria, Iran, Iraq, Sudan, Nigeria, Eritrea, Kyrgyzstan na Myanmar ni miongoni mwa nchi zilizowekwa kwenye orodha hiyo mpya ya kibaguzi.

Ijapokuwa Trump anajaribu kuonyesha kuwa uamuzi huo ni wa kulinda usalama wa taifa la Marekani, lakini kwa hakika unachukuliwa kuwa wa kisiasa na wa kufuatilia malengo ya uchaguzi zaidi kuliko vitisho vya ugaidi. Hasa kwa kutilia maanani kuwa nchi hiyo inajiandaa kufanya uchaguzi wa ndani, hivyo vitendo kama hivyo vinaweza kutathminiwa kama chombo cha kuhamasisha wapiga kura wahafidhina na wenye mielekeo ya utaifa kupigia kura wagombea wa chama tawala. Ukitazama orodha hii unaona kuwa hata nchi nyingi zilizojumuishwa katika orodha hiyo, kama vile Chad, zimekuwa na ushirikiano wa karibu na Marekani kwa miaka mingi katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kile kinachodaiwa kuwa mapambano dhidi ya ugaidi.

Rais Mahamat Idriss Deby wa Chad

Iran, ambayo imekuwa katika orodha ya vikwazo vya visa ya Marekani tangu 2017, kwa mara nyingine tena imeitaja hatua hiyo kuwa mfano wa wazi wa "ubaguzi wa kidini na kikabila," ukiukaji wa uhuru wa kutembea dhidi ya raia wa Iran na kuendelea kwa sera za chuki dhidi ya Uislamu katika sera za kigeni za Marekani. Rais Mahamat Idriss Deby wa Chad pia ametoa tamko la wazi katika taarifa rasmi aliyoituma kwenye mtandao wa kijamii wa X kwa kusema: "Nimeiamuru serikali kuacha kutoa visa kwa raia wa Marekani kwa mujibu wa kanuni ya kulipiza kisasi." Ameongeza kwa maneno ya fahari kuwa: "Chad haina shirika la ndege la kutoa wala mabilioni ya dola, lakini tuna hadhi na heshima yetu."

Katika mahusiano ya kimataifa, kanuni ya kulipiza kisasi ni mojawapo ya kanuni zinazokubalika za kujibu maamuzi ya upande mmoja. Kwa kutumia kanuni hii, Chad imetangaza rasmi kwamba haitafumbia macho siasa zizsizo za kimantiki za Marekani za kutaka kuyafedhehesha mataifa mengine duniani. Nigeria, mojawapo ya nchi zenye watu wengi zaidi barani Afrika na yenye uchumi mkubwa zaidi barani humo, imeutaja uamuzi huo wa Marekani kuwa usio wa haki na unaopingana na moyo wa ushirikiano wa pande mbili. Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imemwita balozi wa Marekani nchi humo ili kumkabidhi malalamiko rasmi ya nchi hiyo kuhusu suala hilo. Nchi za Umoja wa Afrika pia zimeutaja uamuzi huo katika taarifa rasmi kuwa ni wa kibaguzi na ulio kinyume na misingi ya usawa katika mahusiano ya kimataifa.

Ingawa Trump anajaribu kuhalalisha uamuzi huu mbele ya fikra za waliowengi ndani na nje ya Marekani, lakini ni wazi kuwa nchi mbalimbali, hata zile dhaifu, haziko tayari tena kutwishwa sera na matakwa ya Marekani. Maamuzi kama haya yanaweza kuwa na matokeo makubwa hasi kwa taswira ya kimataifa ya Marekani, kupunguza uaminifu kati ya nchi na kutoa changamoto kwa mashirikiano ya kimataifa. Nchi mbalimbali zimetangaza uamuzi huo wa Trump kuwa unadhuru moyo wa ushirikiano wa pande kadhaa, kuchochea ubaguzi na ukiukaji wa kanuni za Hati ya Umoja wa Mataifa. Kwa upande mwingine, nchi za Kiafrika zimeonyesha tena kwamba haziko tayari kufuata kibubusa sera na matakwa ya Marekani ambapo hatua ya kulipiza kisasa ya hivi karibuni ya Chad ni ushahidi wa wazi wa suala hilo.