Aragchi: Iran haitaki kumiliki silaha za nyuklia
(last modified Sat, 07 Jun 2025 13:05:34 GMT )
Jun 07, 2025 13:05 UTC
  • Aragchi: Iran haitaki kumiliki silaha za nyuklia

Seyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amesisitiza kwa mara nyingine kuwa Iran haina nia yoyote ya kumiliki silaha za nyuklia, akieleza kwamba msimamo wa Iran umejengwa juu ya misingi ya kidini pamoja na fatwa ya wazi iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al-Nile News cha Misri, alipokuwa ziarani mjini Cairo tarehe 1 Juni, Aragchi amesema "Hatuna hamu yoyote ya kupata silaha za nyuklia, kwa sababu jambo hili linakinzana na imani zetu za msingi."

“Fatwa ya Ayatullah Khamenei ilitangaza wazi kuwa kumiliki silaha hizo ni haramu, na kwa kuwa sisi ni taifa lenye misingi ya kidini, hatuwezi kuyakiuka maelekezo hayo."

Amefafanua kuwa Tehran inaendelea kushiriki katika mazungumzo ya nyuklia ili kuonesha kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani. Amesema: “Iwapo kuna maswali au mashaka, tuko tayari kuyashughulikia kwa njia ya kujenga imani."

Araghchi amesisitiza kuwa Iran itaendeleza diplomasia na kuwa ina uwezo wa kuonesha nia njema na kujenga uaminifu.

Ameongeza kwamba diplomasia na nia njema ya Iran itazima moja ya madai makuu ya utawala wa Kizayuni.

Ameendelea kusema kwamba: “Tunatambua kikamilifu kwamba utawala wa Kizayuni unamiliki makumi ya silaha za nyuklia, lakini bado unaituhumu Iran kutafuta silaha hizo. Lakini msimamo wetu uko wazi: mpango wetu wa nyuklia ni wa amani na hauna tishio kwa taifa lolote au upande wowote.”

Akigusia matukio ya hivi karibuni katika Bahari Nyekundu, Araghchi amehusisha hali hiyo na mienendo ya kisiasa ya kanda hiyo. “Kinachoendelea katika Bahari Nyekundu ni ishara ya kuungwa mkono wananchi wa Gaza na watu wa Yemen.”

Ameongeza kuwa: “Kulingana na taarifa tulizonazo, meli zilizoandamwa katika Bahari Nyekundu zilikuwa aidha zinamilikiwa na Waisraeli au zilikuwa zikielekea Israel."

Pia amegusia makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kati ya harakati ya Ansarullah ya Yemen na Marekani, na kusema yamechangia katika kuleta “utulivu wa muda katika eneo hilo.”

Katika upande mwingine, mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel pamoja na mzingiro wa Gaza vimesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 54,381 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 124,054, kwa mujibu wa maafisa wa afya wa eneo hilo.

Araghchi pia ameelezea dhamira ya Iran ya kuimarisha mahusiano ya dhati na ya kujenga na mataifa jirani na kanda nzima, hasa mataifa ya Kiarabu.