Wamarekani washiriki kupiga kura katika uchaguzi wa rais wenye mchuano mkali
(last modified Tue, 05 Nov 2024 12:17:40 GMT )
Nov 05, 2024 12:17 UTC
  • Wamarekani washiriki kupiga kura katika uchaguzi wa rais wenye mchuano mkali

Mamilioni ya Wamarekani wamejitokeza kwenye vituo vya kupigia kura kote nchini humo leo Jumanne huku mustakabali wa urais wa nchi hiyo na bunge lake la Kongresi ukiwa hautabiriki.

Makamu wa Rais Kamala Harris wa chama cha Democrat na mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump, wanachuana vikali, huku chunguzi nyingi za maoni zikionyesha kuwa wamepitana kwa asilimia moja hadi tatu tu.
 
Kinyang'anyiro cha urais kinaonekana kuwa kigumu zaidi hasa katika majimbo saba muhimu yanayoathiri matokeo, ambapo mpitano wa wagombea hao wawili katika majimbo manne muhimu ya Nevada, Wisconsin, Michigan na Pennsylvania ni wa asilimia 1 tu au chini ya hapo.
 
Trump, hata hivyo, anaongoza katika  majimbo ya Arizona, Georgia na North Carolina, lakini ni kwa wastani wa chini ya asilimia 3.

Mtandao wa habari wa Bloomberg umesema, uchaguzi wa rais wa mwaka 2024 nchini Marekani unachukuliwa kuwa ni wa kushangaza zaidi katika miongo ya hivi karibuni kwa matukio yaliyojiri ndani yake hadi sasa, ambapo kwa upande mmoja wameshuhudiwa Wademokrasia wakibadilisha mgombea wao, ambaye ni Rais Joe Biden; na kwa upande mwingine, mgombea urais wa Republican Donald Trump alishambuliwa kwa risasi wakati wa kampeni.

 
Kwa mujibu wa Bloomberg, katika uchaguzi huu, ikiwa Harris atashinda, atakuwa mwanamke wa kwanza mweusi na wa Asia kuwa rais wa Marekani, na ikiwa Trump atashinda, atakuwa mgombea aliyerejea White House kwa mara ya pili.../