China yakanusha kukabiliana na ugonjwa unaoshabihiana na Uviko-19
(last modified Sun, 05 Jan 2025 07:43:20 GMT )
Jan 05, 2025 07:43 UTC
  • China yakanusha kukabiliana na ugonjwa unaoshabihiana na Uviko-19

China imekadhibisha madai kwamba inakabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kupumua usiofahamika unaofanana na Uviko-19.

Mao Ning, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameeleza kuwa maambukizi yaliyoripotiwa nchini humo ni kesi za homa ya mafua inayohusiana na msimu wa baridi kali.

Mao amesema kuwa, maambukizi ya mfumo wa kupumua huwa yanaongezeka wakati wa msimu wa baridi kali katika Ukanda wa Kaskazini na kwamba mafua haya si makali na yanaenea kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Tarehe Mosi mwezi huu wa Januari kulisambaa mitandaoni video zikionyesha idadi kubwa ya wagonjwa huku hospitali za China zikiwa zimezidiwa kwa wagonjwa waliofika kupatiwa huduma. Video hizo ziliwaonyesha wauguzi na madaktari wakiwa katika sare za kujikinga na maambukizi huku watu wa kawaida wakiwa wamevaa barakoa.

Huku haya yakijiri, Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani hadi sasa kimekadiria kuwepo wagonjwa wa mafua wasiopungua milioni 5.3, 63 ambao wamelazwa hospitalini na 2,700 wamepoteza maisha kwa homa ya mafua.