China: Hatuogopi kupigana vita vya kibiashara na Marekani
(last modified Thu, 17 Apr 2025 02:29:16 GMT )
Apr 17, 2025 02:29 UTC
  • China: Hatuogopi kupigana vita vya kibiashara na Marekani

China imeonya kwamba "haiogopi" kupigana vita vya kibiashara na Marekani, ikikariri wito wa mazungumzo baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kusema kwamba Beijing lazima ichukue hatua ya kwenda kwenye meza ya mazungumzo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian amesema ikiwa Marekani inataka kweli kutatua suala hilo kwa njia ya mazungumzo na diplomasia, inapaswa kuacha kutoa mashinikizo, vitisho na uhasama; na izungumze na China kwa misingi ya usawa, heshima na manufaa ya pande zote mbili.

"Msimamo wa China umekuwa wazi sana. Hakuna mshindi katika vita vya ushuru au vita vya biashara," amesema Jian na kuongeza kuwa, "China haitaki kupigana, lakini pia haiogopi kupigana."

Matamahi hayo ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China yametolewa huku utawala wa Trump ukiweka ushuru mpya wa forodha kwa wapinzani na hata washirika wa Marekani, lakini hatua zake hizo zimeilenga zaidi China.

Wachumi wameonya kuwa, ushuru wa Trump dhidi ya China na hatua za kukabiliana na Beijing zinatarajiwa kupunguza biashara kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa zaidi duniani kutoka kilele chake cha hivi karibuni cha karibu dola bilioni 700 kwa mwaka hadi karibu sufuri.

Ikulu ya Rais wa Marekani ilitangaza hivi karibuni kwamba, bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka China sasa zitatozwa ushuru wa asilimia 145, na huenda ukapindukia asilimia 200.

Mbali na kujibu mapigo kwa hatua hizo za serikali ya Trump, serikali ya Beijing imeyaweka makampuni sita ya Kimarekani katika orodha ya mashirika yasiyoaminiwa na wakati huo huo imezidisha jitihada za kidiplomasia za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN).