WHO yasikitishwa na Marekani kujiondoa kwenye shirika hilo
(last modified Wed, 22 Jan 2025 02:49:43 GMT )
Jan 22, 2025 02:49 UTC
  • WHO yasikitishwa na Marekani kujiondoa kwenye shirika hilo

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeelezea masikitiko yake kufuatia tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuiondoa nchi hiyo kwenye shirika hilo. WHO imesema inatumai serikali mpya ya Washington itaangalia upya uamuzi wake huo.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne, shirika hilo limesisitiza kuwa, lina jukumu muhimu katika kulinda afya na usalama wa kimataifa, ikwemo afya na siha wa wananchi wa Marekani.

Marekani ambayo imekuwa mchangiaji mkubwa zaidi wa bajeti ya shirika la WHO imedai kuwa, itaelekeza mchango huo katika mashirika mengine ambayo yanajishughulisha na masuala ya afya na usalama wa jamii duniani. Hatua hiyo ya Trump imekabiliwa na lawama kali za ndani na nje ya nchi. 

Katika muhula wake wa kwanza, Trump mbali na kulilaumu shirika la WHO eti kwa kushindwa kukabiliana na tandavu ya COVID-19, alidai kuwa, taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inadhibitiwa na China; na kuamua kuikatia misaada yote ya kifedha.

Wakati huo huo, Guo Jiakun, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema kwamba, jukumu la Shirika la Afya Duniani (WHO) linapaswa kuimarishwa, sio kudhoofishwa, na kwamba China itaendelea kuunga mkono WHO katika kutekeleza majukumu yake.

Guo amesisitiza kuwa, China, kama kawaida, itaunga mkono WHO katika kutekeleza majukumu yake, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wa afya ya umma, kuimarisha mifumo ya afya duniani, na kuhimiza juu ya kustawishwa jumuiya ya kimataifa ya afya kwa wote.