Je Magharibi inakabiliwa na mporomoko?
Zilzala iliyoibuliwa na Trump kwa kujikurubisha kwa Russia ili kuhitimisha vita huko Ukraine imeambatana na chambuzi mbalimbali kuhusu suala la umoja kati ya Marekani na Ulaya.
Trump amepuuza nafasi ya serikali ya Ukraine na ya Ulaya kwa ujumla, na kuingia katika mazungumzo ya moja kwa moja na Russia na kuhoji muundo wa uhusiano wa panden mbili wa nchi za Atlantiki baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia.
Kwa miaka mingi baada kusambaratika Umoja wa Kisovieti, huko Ulaya na katika nchi za Magharibi ilifikiriwa kwamba katika mfumo mpya utakaoundwa; mifumo ya Demokrasia Huria ya Magharibi ingeungana na kuwa na umoja madhubuti mkabala wa mifumo ya serikali kuu inayopinga sera za Magharibi. Hata hivyo baada ya kuingia madarakani Donald Trump huko Marekani na kudhihirisha wazi misimamo yake na timu inayomuunga mkono dhana hiyo imebatilika.
Gazeti la New York Times limeandika katika ripoti yake ya karibuni kuhusu suala hili kwamba: Bado haijafahamika kuhusu hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kujikurubisha kwa Russia na kuwatelekeza waitifaki wao wa muda mrefu itaendelea hadi lini. Lakini yumkini Magharibi imesambaratika.
Waraka wa New York Times umeashiria namna nchi za Ulaya zinavyopambana na zama mpya na kuripoti kuwa, Marekani sasa imeamua kumpa kisogo mshirika wake na badala yake imejikurubisha kwa Rais Vladimir Putin wa Russia. Ripoti hiyo ya New York Times imeongeza kwamba: Ulaya ambayo inahisi kutengwa ina wasiwasi kuhusu jukumu kubwa lililo mbele yake la kujizatiti upya kwa silaha, na imeshangazwa na mabadiliko ya aidiolojia ya Marekani.
Valerie Hayer Mkuu wa Kundi la The European Renewal Group katika bunge la Ulaya amesema: "Marekani ilikuwa nguzo ambayo amani ilisimamiwa, lakini imebadilisha muungano uliokuwepo. Trump anakariri propaganda za Putin. Tumeingia katika zama mpya". Jarida la Foreign Policy pia limeashiria hatua ya karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani na kuandika: Serikali ya Trump imechukua hatua zaidi ya kutazama upya suala la Muungano wa Atlantiki; Marekani sasa amekuwa adui wa Ulaya.
Jarida hilo la nchini Marekani limeongeza kuwa: Inaonekana kuwa Trump amebadili msimamo wake ambapo sasa anamuona Rais wa Russia kama chaguo bora la muda mrefu badala ya kuzitambua nchi za Ulaya kama washirika muhimu zaidi wa Marekani. Katika hali ambayo kwa miaka kadhaa sasa kumekuwepo na uvumi kuhusu hamu ya Trump ya kujikurubisha kwa Putin; hivi sasa inaonekana kuwa hisia hizi za pamoja ndizo zinazoongoza sera ya Marekani.
Waliopoteza au kushindwa pakubwa kutokana na mabadiliko ya Trump mkabala wa washirika wake ni nchi za Ulaya ambazo kwa muda wa miaka 80 zimekuwa chini ya mwavuli wa usalama wa Marekani. Hii ni katika hali ambayo serikali za Ulaya zenyewe zinakabiliwa na changamoto kubwa ndani na katika ngazi ya Umoja wa ulaya kwa ajili ya kujidhaminia usalama wao. Nicole Bacharan, Profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Po huko Paris anasema: "Bila kujali mabadiliko ya kimbinu ya Trump, hatari kubwa zaidi ni kukana kwamba ameacha demokrasia huria." Trump anajua anakokwenda. Msimamo pekee wa kweli kwa Ulaya ni huu unaohoji: Je, tuna nguvu gani ya kijeshi na tunawezaje kuunganisha na kuimarisha nguvu hii haraka iwezekanavyo?
Hakuna nchi barani Ulaya ambayo imeyumbishwa na mabadiliko ya mtazamo wa Marekani kama Ujerumani. Jamhuri ya Ujerumani ya baada ya vita iliundwa kwa kiasi kikubwa kwa msaada wa Marekani. Ujerumani ni mwenyeji wa wanajeshi 35,000 wa Marekani na makumi ya silaha za nyuklia.
Haya yanajiri huku kukiwa na uvumi kwamba Marekani inapanga kuwaondoa wanajeshi wake huko Ujerumani na kuwahamishia Hungary. Matukio haya yote yanaashiria mabadiliko makubwa ya kimkakati.