Mjumbe wa Marekani: Rais Zelensky wa Ukraine ameomba msamaha kwa Trump
Mar 11, 2025 23:04 UTC
Mjumbe maalumu wa Marekani katika Mashariki ya Kati Steve Witkoff amesema, Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky ameomba msamaha kwa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusiana na sakata lililozuka baina yao wakati wa mkutano kwenye Ikulu ya White House.
Witkoff ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya Fox News, kabla ya mkutano kati ya wajumbe wa Marekani na Ukraine unaofanyika nchini Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo wa Marekani katika Mashariki ya Kati, Washington inatarajia kupata "maendeleo makubwa" na inatumai kuwa itasaini makubaliano muhimu sana ya madini na Kiev.
"Zelensky alituma barua kwa rais. Aliomba msamaha kwa tukio zima lililotokea katika Ofisi ya Oval," ameeleza Witkoff na kuongezea kwa kusema: "nadhani ilikuwa hatua muhimu na kumekuwa na majadiliano mengi kati ya timu zetu na Waukraine na watu wa Ulaya ambao wana umuhimu pia kwa ajil ya majadiliano haya".
Hivi karibuni, Trump alifichua kuwa wiki iliyopita, alipokea barua "muhimu" kutoka kwa Zelensky inayoelezea utayarifu wa Kiev wa "kuja kwenye meza ya mazungumzo haraka iwezekanavyo".
Hata hivyo rais huyo wa Marekani hakutaja kama barua hiyo ilikuwa ndani yake ina ujumbe pia wa kuomba msamaha kwa sakata lililozuka kwenye Ofisi ya Oval.
Zelensky alipapurana kwa makelele na maneno makali na Trump na Makamu wake JD Vance wakati wa mazungumzo kwenye Ikulu ya White House mwezi uliopita. Rais wa Marekani alimtuhumu mwenzake wa Ukraine kwamba hakuonyesha heshima na shukurani kwa misaada iliyotolewa Marekani, ni mwenye shaka katika kufikia amani na Russia na "anacheza kamari na Vita vya Tatu vya Dunia".
Zelensky alitakiwa aondoke Ikulu ya White House kabla mazungumzo ya faragha baina yake na Trump kuanza.../