Marekani yapanga kuishambulia kijeshi Panama
https://parstoday.ir/sw/news/world-i123896-marekani_yapanga_kuishambulia_kijeshi_panama
Panama imesisitiza kujitolea kwake kudumisha uhuru wake kufuatia ripoti kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump, anatafakari kuchukua hatua za kijeshi kudhibiti 'Mfereji wa Panama'.
(last modified 2025-03-14T03:23:11+00:00 )
Mar 14, 2025 03:23 UTC
  • Marekani yapanga kuishambulia kijeshi Panama

Panama imesisitiza kujitolea kwake kudumisha uhuru wake kufuatia ripoti kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump, anatafakari kuchukua hatua za kijeshi kudhibiti 'Mfereji wa Panama'.

Kituo cha habari cha NBC kiliripoti Alhamisi kuwa Ikulu ya White House iliagiza jeshi la Marekani kuandaa mipango ya "kurejesha" mfereji huo mikononi mwa Marekani. Kwa mujibu wa maafisa wawili wa Marekani waliopo kwenye mipango hiyo, Ikulu ilitoa maagizo kwa jeshi kuongeza uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Panama ili kutimiza lengo la Trump la kudhibiti tena mfereji huo.

Katika kujibu ripoti hizo, serikali ya Panama imesitiza kuwa itabaki "imara" katika kutetea uhuru wake na Mfereji wa Panama.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Panama, Javier Martinez-Acha, akizungumza na waandishi wa habari amesema:"Kuhusu matamshi haya, sina la kuongeza zaidi ya kwamba Panama inasalia imara katika kutetea ardhi yake, mfereji wake, na mamlaka yake."

Aliendelea kusisitiza kwamba: "Mfereji huu ni mali ya Wapanama, na utaendelea kuwa hivyo."

Inaripotiwa kuwa lengo la utawala wa Trump ni kuongeza uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Panama ili kupunguza ushawishi wa China, hasa uwezo wake wa kutumia njia hiyo ya kimkakati ya meli za biashara.

Pia, katika hotuba yake kwa Bunge la Marekani wiki iliyopita, Trump alisisitiza kuwa "ili kuimarisha zaidi usalama wa taifa letu, utawala wangu utarejesha Mfereji wa Panama."

Kwa sasa, inaripotiwa kuwa Marekani ina zaidi ya wanajeshi 200 nchini Panama, ingawa idadi hiyo hubadilika kutokana na mzunguko wa vikosi vinavyoingia na kutoka.

Marekani ilichukua rasmi ujenzi wa mfereji huo kutoka kwa Ufaransa mwaka 1904, na baada ya miaka 10, mfereji huo ulianza kufanya kazi chini ya udhibiti wa Marekani. Hata hivyo, mwaka 1999, Marekani ilikabidhi rasmi mfereji huo kwa Panama.

Mfereji wa Panama ni njia ya maji yenye urefu wa kilomita 82 inayounganisha Bahari ya Karibea na Bahari ya Pasifiki.