Zelenskyy: Ukraine imepokea pendekezo jipya la Marekani kuhusu makubaliano ya madini
(last modified Sun, 30 Mar 2025 02:37:10 GMT )
Mar 30, 2025 02:37 UTC
  • Zelenskyy: Ukraine imepokea pendekezo jipya la Marekani kuhusu makubaliano ya madini

Rais wa Ukraine amesema kuwa Kiev imepokea pendekezo jipya kutoka Marekani kuhusu makubaliano ya madini.

Rais Volodymyr Zelenskyy amesema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa pendekezo jipya llilotolewa na Marekani ni tofauti sana na pendekezo la awali la nchi hiyo kuhusu madini, na kusisitiza kuwa suala hili ambalo tayari limewasilishwa rasmi katika ofisi yake, litachunguzwa na kulinganishwa na pendekezo la awali la Washington katika uwanja huo.  

Zelenskyy kwa mara nyingine tena amepinga dhana kwamba misaada ya kijeshi ya Marekani kwa Ukraine ni lazima ihesabiwe kama mkopo. 

Itakumbukwa kuwa, wiki kadhaa zilizopita mkutano wa Zelenskyy na mwenzake wa Marekani, Donald Trump katika Ofisi ya Oval, ambao ulipangwa kukamilisha makubaliano ya kuipatia Marekani haki ya madini adimu ya Ukraine, uligeuka na kuwa vuta nikuuvute ya maneno baina ya marais wa Marekani na Ukraine.

Malumbano baina ya Zelenskyy na Trump, White House

Rais wa Ukraine pia ameeleza kuwa nchi hiyo inajiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa ngazi ya juu wa wawakilishi wa kijeshi wa nchi zilizo tayari kutuma wanajeshi nchini Ukraine. Ufaransa, Uingereza na mwenyeji Ukraine zimethibitisha kushiriki katika mkutano. 

Ameongeza kuwa vifurushi vipya vya misaada ya kiulinzi vitatangazwa mwezi Aprili katika mkutano ujao utakaofanyika katika kambi ya Rammstein. 

Inafaa kuashiria hapa kuwa, vita vya Ukraine vilianza baada ya nchi za Magharibi kupuuza wasiwasi wa usalama wa Moscow na kisha kupanua uwepo vikosi vya Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO karibu na mipaka ya Russia.