Ubelgiji nayo yatia ulimi puani, yasema: Hatutamkamata Netanyahu
Apr 09, 2025 03:05 UTC
Ubelgiji nayo pia imetangaza kuwa haitotii amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ya kutaka waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu akamatwe na kukabidhiwa kwa mahakama hiyo.
Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever ametetea hatua hiyo alipokuwa akizungumza katika mahojiano na shirika la habari la nchi hiyo la VRT.
De Wever ametamka bayana kuwa Ubelgiji haitamkamata Netanyahu ikiwa ataitembelea nchi hiyo.
"Kuna kitu kiitwacho siasa za uhalisia wa mambo. Mazingatio ya kiutendaji yanashinda mazingatio ya kimaadili", ameeleza waziri mkuu huyo wa Ubelgiji.
Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, Mahakama ya ICC yenye makao yake The Hague ilitoa hati za kukamatwa Netanyahu na waziri wake wa vita wa wakati huo Yoav Gallant kwa kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita unaofanywa huko Ghaza. Licha ya kukabiliwa na tishio hilo la kukamatwa, Netanyahu ameshatembelea Marekani na Hungary na kutumia anga ya Ufaransa.
Kadhalika, De Wever ameieleza VRT kwamba, nchi nyingi za Ulaya pia zitakaidi agizo la Mahakama ya Kimataifa ya Jinai la kumkamata Netanyahu na akabainisha kwa kusema: "Ufaransa haitafanya, na sidhani kama na sisi tutafanya hivyo" , huku akidai kwamba kutekeleza amri hiyo ya kumkamata waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni ni jambo lisilowezekana.
Wachambuzi wa siasa za Ulaya wanautathmini msimamo huo wa Ubelgiji kuwa ni kielelezo kingine cha sera za undumakuwili na za kinafiki zinazokinzana na madai ya nchi za Magharibi ya kutetea haki na sheria za kimataifa.../
Tags