Marekani yaendeleza mradi wa kuwatimua wanafunzi wa kimataifa wanaoiunga mkono Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i125048-marekani_yaendeleza_mradi_wa_kuwatimua_wanafunzi_wa_kimataifa_wanaoiunga_mkono_palestina
Ukandamizaji na vitisho dhidi ya wanafunzi wanaounga mkono haki ya Wapalestina unaendelea katika vyuo vikuu vya Marekani, jambo ambalo limevuruga mfumo wa elimu nchini humo.
(last modified 2025-04-11T22:48:08+00:00 )
Apr 11, 2025 22:48 UTC
  • Marekani yaendeleza mradi wa kuwatimua wanafunzi wa kimataifa wanaoiunga mkono Palestina

Ukandamizaji na vitisho dhidi ya wanafunzi wanaounga mkono haki ya Wapalestina unaendelea katika vyuo vikuu vya Marekani, jambo ambalo limevuruga mfumo wa elimu nchini humo.

Mamia ya wanafunzi wa kimataifa na makumi ya vyuo vikuu kote Marekani wamekuwa waathirika wa sera ya utawala wa Donald Trump inayolenga kukandamiza wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina. Wanafunzi wa kimataifa wamekuwa wakifutiwa viza zao hata kwa makosa madogo kama kosa la trafiki. Vyuo vikuu pia vimeamrishwa kuchunguza taarifa za uhamiaji ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wao bado wana haki ya kubaki nchini.

Jarida la The Hill likinukuu tovuti ya Marekani ya Inside Higher Ed, linaripoti kuwa zaidi ya vyuo na vyuo vikuu 80 vimekumbwa na kesi za kufutwa kwa viza za wanafunzi wao.

Katika wakati ambapo Marekani hujigamba kama mtetezi wa uhuru wa kisiasa, kijamii na haki za binadamu duniani, ukandamizaji huu dhidi ya wanafunzi unaonyesha unafiki wa madai hayo – hasa tangu kuingia madarakani kwa Trump. Vyuo na wanafunzi nchini Marekani wamekuwa wakishinikizwa sana, wengine wakitishiwa kukatiwa ufadhili iwapo hawatatii sera za serikali, hasa kuhusu Palestina.

Sio tu uhuru wa kujieleza ambao umelengwa; bali hata misingi ya kielimu na kibinadamu ya taasisi hizi imewekwa mashakani. Wanafunzi wa kimataifa – wengi wao wakiwa ni wafuasi wa harakati za kupigania Palestina – wamewekwa chini ya usimamizi mkali. Visa vya kufutwa kwa viza, vitisho vya kufukuzwa, na kufuatiliwa kwa shughuli zao za kijamii na kisiasa ni sehemu ya mchakato huu ulioenea katika vyuo zaidi ya 80.

Wanafunzi nchini Marekani katika maandamano ya kuunga mkono Palestina

Miriam Feldblum, rais wa Chama cha Wakuu wa Vyuo vya Elimu ya Juu, ameeleza kuwa kukosekana kwa mwelekeo wazi kutoka kwa serikali ya Trump na kupuuzwa kwa mchakato wa kisheria kumeziweka taasisi za elimu katika hali ya hatari.

Hili si jambo jipya: historia ya vyuo vikuu vya Marekani imejaa matukio ya ukandamizaji dhidi ya wanafunzi wanaopinga sera za serikali. Mwaka 1968, katika Chuo Kikuu cha Columbia, serikali ilitumia wanajeshi kukabiliana na wanafunzi waliposhiriki mgomo kulalamikia ushiriki wa chuo kwenye miradi ya kijeshi, na sera za serikali ya wakati huo ya kuendeleza vita dhidi ya Vietnam na kuunga mkono utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Serikali ilitumia maafisa wa polisi na gadi ya taifa kuwapga na kuwakamta wanafunzi. Hali hii imejirudia tena na tena – kutoka maandamano dhidi ya vita vya Iraq hadi mikusanyiko ya kuunga mkono Palestina katika miaka ya karibuni.

Leo, wanafunzi wanaothubutu kueleza mshikamano wao na watu wa Palestina na kulaani uvamizi wa Israel huko Gaza wanakabiliwa na adhabu kali.

Ukimya wa vyuo vikuu vingi mbele ya wimbi hili jipya la ukandamizaji unaashiria mmomonyoko wa maadili katika mfumo wa elimu ya juu Marekani. Vyuo vingi vinachagua kunyamaza au hata kushirikiana na serikali kwa hofu ya kupoteza msaada wa kifedha au kukumbwa na mashinikizo la kisiasa. Katika hali hii, wanafunzi wa kimataifa – hasa kutoka Asia na Afrika – wanakumbwa na dhuluma ya kipekee. Jambo hili linaonyesha wazi ubaguzi wa rangi ulioko hata ndani ya mfumo wa elimu nchini Marekani.

Kwa kweli, ukandamizaji wa wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina hauwezi tena kuonekana tu kama mzozo wa kielimu au uhamiaji – bali ni ishara ya kusambaratika kwa madai ya kimaadili, kibinadamu, na kiutamaduni ya Magharibi, hasa Marekani.