Wanafunzi Waislamu Ulaya walaani mauaji ya watoto Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/world-i12514-wanafunzi_waislamu_ulaya_walaani_mauaji_ya_watoto_yemen
Muungano wa vyama vya wanafunzi wa Kiislamu barani Ulaya umemuandikia barua Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ukitaka hatua za makusudi zichukuliwe kukomesha mauaji ya raia wasio na hatia na hususan watoto wadogo nchini Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 03, 2016 02:55 UTC
  • Wanafunzi Waislamu Ulaya walaani mauaji ya watoto Yemen

Muungano wa vyama vya wanafunzi wa Kiislamu barani Ulaya umemuandikia barua Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ukitaka hatua za makusudi zichukuliwe kukomesha mauaji ya raia wasio na hatia na hususan watoto wadogo nchini Yemen.

Katika barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa UN, wanafunzi hao wa Kiislamu barani Ulaya wameutaka umoja huo na jamii ya kimataifa kwa ujumla zishinikize kuchukuliwa hatua kali watawala wa Aal-Saud kutokana na mashambulizi ya anga ya jeshi la utawala huo, yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 9,400 hadi sasa nchini Yemen.

Kwa mujibu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen, Saudi Arabia imeua watoto karibu 2,000 wa Yemen na kuvunja haki za maelfu ya wengine katika hujuma zake.

Wanafunzi Waislamu Ulaya

Aidha muungano huo wa vyama vya wanafunzi wa Kiislamu barani Ulaya umekosoa kimya cha jamii ya kimataifa, watetezi wa haki za binadamu na vyombo vya habari vya Magharibi kwa kuyafumbia macho mauaji hayo ya watoto Yemen.

Mapema jana ndege za kijeshi za Aal-Saud zilifanya mashambulizi ya anga na kulenga majengo ya raia katika kijiji cha al-Shamil, wilaya ya Wuday mkoani Abyan na kuua watoto watatu na kujeruhi vibaya wazazi wao.

Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Ban Ki-moon anaendelea kukabiliwa na mashinikizo ya kila upande baada ya kuiondoa Saudia kwenye orodha nyeusi ya Umoja wa Mataifa ya wakiukaji wa haki za watoto, kutokana na kushambulia vituo na makazi ya raia na kuua mamia ya watoto wadogo wa Yemen.