Trump apinga marekebisho ya sheria ya haki ya kubeba silaha
Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kuwa hana mpango wa kufanyia marekebisho sheria ya haki ya kubeba silaha nchini humo licha ya kushuhudia mara kwa mara ufyatuaji risasi mashuleni na katika vituo vya elimu nchini humo.
Trump ameeleza haya licha ya tukio la ufyatuaji risasi wa kutisha katika Chuo Kikuu cha jimbo la Florida ambapo ametoa mkono wa pole kwa wahanga wa hujuma hiyo.
Maafisa husika wa Marekani wametangaza kuwa, mtoto wa kiume wa Naibu Mkuu wa Polisi ndiye mshukiwa wa mauaji ya watu wawili katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Florida mapema wiki hii.
Ufyatuaji risasi huo umetokea kaskazini mwa jimbo la Florida mahali alipozaliwa Rais Donald Trump wa Marekani. Licha ya kueleza masikitiko yake kufuatia shambulio hilo la risasi, lakini Trump ametangaza kuwa hana mpango wa kubadili sheria ya haki ya kumiliki silaha huko Marekani.
Aghalabu ya wahafidhina wa chama cha Repubican wanauona umiliki wa bunduki kama haki muhimu ya mtu na isiyoweza kujadiliwa. Hata hivyo katika hali ambayo Marekani inakakabiliwa na uhalifu mkubwa wa kutumia bunduki katika maeneo ya umma, Wademocrat kwa upande wao wanashinikiza kuwepo kwa sheria kali zaidi ili kudhibiti matumizi ya silaha.