Waandamanaji 330 watiwa mbaroni Los Angeles Marekani
Msemaji wa Ikulu ya Marekani amezungumzia hali ya mji wa Los Angeles baada ya kuzuka maandamano makubwa ya wananchi dhidi ya sera za uhamiaji za utawala wa Trump na kuosema kuwa, hadi hivi sasa wahajiri 330 wametiwa mbaroni mjini Los Angeles (pekee) ikiwa ni sehemu ya kukandamiza kilio cha wananchi.
Msemaji wa Ikulu ya White House, Caroline Leavitt amesema kuwa, tangu siku ya Ijumaa hadi hivi sasa, waandamanaji 330 wameshatiwa mbaroni huko Los Angeles (pekee).
Katika hatua ya ukandamizaji na inayokinzana na madai ya demokrasia na haki ya kujieleza, rais wa Marekani Donald Trump ametuma zaidi ya wanajeshi 4,000 wa Gadi ya Taifa na wanajeshi 700 wa Jeshi la Majini la Marekani (Marines) huko Los Angeles kwa lengo la kukandamizaji waandamanaji wasio na silaha.
Kabla ya hapo Gavana wa Jimbo la California, Gavin Newsom alimuonya Trump kuhusu hatua zake za kutia mbaroni watu na kusema kuwa, itachochea mgawanyiko. Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, maandamano ya Los Angeles yamechochewa na ukandamizaji wa Trump na sera zake za kidikteta dhidi ya wahamiaji.
Baada ya Gavana wa Calipofornia kulalamikia udikteta wa Trump wa kupeleka jimboni humo wanajeshi wa Gadi ya Taifa bila ya kumshauri, rais huyo wa Marekani hakurudi nyuma, bali aliamuru Jumatatu jioni kupelekwa mamia ya wanajeshi wa Jeshi la Majini la Marekani (Marines) kwenda kukandamiza waandamanaji.
Katika upande mwingine, msemaji wa Ikulu ya White House amekataa kutoa maelezo yoyote kuhusu barua kutoka kwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Christie Noem, ambaye inadaiwa ameitaka wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon kukabiliana kijeshi na waandamanaji.
Televisheni ya CNN ya Marekani imetangaza kuwa kutiwa mbaroni waandamanaji kunakofanywa na majeshi ya Marekani bila ya kutumia "Sheria ya Machafuko" kunaweza kuwa ni kukiuka sheria ya shirikisho.