UK: Biashara na Ulaya ni muhimu zaidi kwetu kuliko Marekani
(last modified Sun, 27 Apr 2025 02:31:24 GMT )
Apr 27, 2025 02:31 UTC
  • UK: Biashara na Ulaya ni muhimu zaidi kwetu kuliko Marekani

Waziri wa Hazina wa Uingereza, Rachel Reeves amesemaa kuwa, biashara baina ya nchi yake na Umoja wa Ulaya ni muhimu zaidi kuliko uhusiano wa kiuchumi na Marekani.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Reuters la ufalme wa Uingereza ambalo limechapisha makala inayomnukuu Rachel Reeves akisema siku ya Ijumaa kwamba: "Ninaelewa kwamba uhusiano wetu wa kibiashara na Marekani ni muhimu, lakini uhusiano wetu wa kibiashara na Ulaya ni muhimu zaidi kwa sababu nchi za Ulaya ni majirani zetu walioko karibu na mipaka yetu na ni washirika wetu wa jadi wa kibiashara."

Wiki hii Reeves amekutana na mawaziri wa fedha wa Ufaransa, Ujerumani, Uhispania, Poland, Sweden na Finland ili kufufua uhusiano wa kibiashara baina ya Uingereza na Ulaya.

Waziri huyo wa Hazina wa Uingereza pia alikutana na Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Besant mjini Washington siku ya Ijumaa na kujadiliana naye makubaliano ya kibiashara ya nchi hizo mbili.

Reeves amesema katika taarifa fupi kwenye mitandao ya kijamii kwamba: "Uhusiano wa Uingereza na Marekani umepelekea kustawi biashara  katika pande zote za Atlantiki lakini uhusiano wetu na Ulaya ni muhimu zaidi." 

Uingereza, sawa na nchi nyingine, inapigania kupunguza athari za vita vya ushuru vilivyoanzishwa na Marekani, hasa mauzo ya magari ya Uingereza na metali. Nchi hizo zimesaini kusaini makubaliano ya kiuchumi na kuongeza uwekezaji katika teknolojia.

Lakini, Reeves alisisitiza wiki iliyopita kwamba Uingereza haina haraka ya kufikia makubaliano na Marekani na kwamba inastahabu kuwa na uhusiano mzuri zaidi na Ulaya kuliko Washington.