Katibu Mkuu wa UN: Hali ya maafa katika Ukanda wote wa Ghaza imevuka kiwango cha kutasawirika
(last modified Wed, 30 Apr 2025 03:19:36 GMT )
Apr 30, 2025 03:19 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN: Hali ya maafa katika Ukanda wote wa Ghaza imevuka kiwango cha kutasawirika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema: "hali ya kibinadamu katika eneo lote la Ukanda wa Ghaza imetoka kwenye hali mbaya na kuwa mbaya zaidi na kuvuka kiwango cha kuweza kutasawirika".

Guterres ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la UN kilichoitishwa kujadili hali ya Mashariki ya Kati na akaongezea kwa kusema: "kanda ya Mashariki ya Kati inapitia mabadiliko ya kimsingi kutokana na matukio ya kikatili yanayojiri na kuvurugika kwa uthabiti. Kwa karibu miezi miwili kamili, Israel imezuia chakula, mafuta, dawa na vifaa vya kibiashara, na kuwakosesha misaada muhimu sana ya kimaisha zaidi ya Wapalestina milioni mbili katika Ukanda wa Ghaza".
 
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amebainisha kwamba, mapigano na uharibifu usiosita unaendelea kufanywa katika Ukanda wa Ghaza katika hali ya maisha isiyo ya kibinadamu hata chembe ambayo wamehimilishwa nayo watu wa eneo hilo; watu ambao wamekuwa wakishambuliwa mara kwa mara, wanaofungiwa katika maeneo madogo na madogo zaidi na kunyimwa misaada muhimu sana ya kimaisha.
 
Guterres amesisitiza kuwa, Ghaza ni sehemu isiyotenganishika na nchi ya baadaye ya Palestina na ni lazima ibaki kuwa sehemu yake, nalo Baraza la Usalama, kwa kufuata sheria za kimataifa, limekataa jaribio lolote la kubadilisha muundo wa idadi ya watu au ukubwa wa eneo la Ukanda wa Ghaza, ikiwa ni pamoja na hatua yoyote ambayo italipunguza eneo lake.
 
Katika hotuba yake hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kuwa hakuna dalili ya mwisho wa mauaji na mateso katika Ukanda wa Ghaza na akasema, hali ya kibinadamu katika ukanda huo “imebadilika kutoka mbaya, mbaya zaidi hadi ya jinamizi isiyotasawirika”.

Ameongeza kuwa, kwa takribani miezi miwili mfululizo, Israel imezuia chakula, mafuta, dawa na bidhaa nyingine muhimu za kibiashara, ikiwanyima zaidi ya watu milioni mbili misaada ya kuokoa maisha huku dunia ikikodolea macho tu hali hiyo.../