Utendaji tata wa Trump katika siku 100 za kwanza za urais wake
Zimepita siku 100 tangu Donald Trump aingie Ikulu ya White House nchini Marekani.
Taasisi ya uchunguzi wa maoni ya Ipsos imetoa matokeo ya uchunguzi mpya unaoonyesha kuwa, kuridhika kwa Wamarekani na utendaji kazi wa Trump katika siku 100 za kwanza za uongozi wake ni kiwango cha chini zaidi ikilinganishwa na rais yeyote katika miaka 70 iliyopita nchini humo.
Uchunguzi wa maoni wa Ipsos ulihusisha masuala mbalimbali - kuanzia mfumuko wa bei na uhamiaji hadi kodi na utawala wa sheria – ambapo idadi ya Wamarekani wasioridhika na utendaji wa Trump ilizidi wale walioridhika katika masuala haya yote. Hata katika suala la uhamiaji, ambalo linachukuliwa kuwa hatua kali ya Trump, ni asilimia 45 tu ndio waliounga mkono utendakazi wake, huku asilimia 46 wakipinga.
Matokeo ya kura hii ya maoni yanadhihirisha mgawanyiko mkubwa wa kichama katika mitazamo ya nia ya Trump; kiasi kwamba Wademokrat wana uwezekano mkubwa zaidi kuliko Warepublican kuona matamshi ya Trump kama tishio la kweli. Kura mpya ya maoni ya CNN pia ilionyesha kuwa ni asilimia 22 tu ya Wamarekani wanaidhinisha kwa dhati utendaji wa Trump kama rais, kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea, huku takriban mara mbili ya idadi hiyo, asilimia 45, wakipinga vikali utendakazi wake.

Kwa mujibu wa utafiti huo, kiwango cha umaarufu wa Trump kimefikia asilimia 41 ndani ya siku 100 za kwanza za urais wake, kiwango cha chini zaidi miongoni mwa marais wapya wa Marekani katika kipindi cha angalau miongo saba iliyopita, hata ikilinganishwa na muhula wake wa kwanza. Kuridhika kwa wananchi na utendaji wa Trump kumeanguka kwa alama nne ikilinganishwa na mwezi Machi, na kushuka kwa alama saba kutoka mwishoni mwa Februari.
Utafiti mwingine wa New York Times na Siena College umebaini kuwa, wapiga kura wa Marekani wanaamini Trump amechupa mipaka katika jaribio lake la kupanua mamlaka ya utawala wa rais. Pia, wapiga kura wanamuona Trump kama kiongozi asiyeelewa matatizo ya kila siku ya raia wake, hali ambayo imezidisha hasira dhidi ya utawala wake. Katika karibu kila suala kuu, umaarufu wa Trump umeendelea kuporomoka, na imani ya umma katika uwezo wake wa kushughulikia masuala haya muhimu inazidi kuyumba.
Katika siku 100 za kwanza, Trump amechukua hatua nyingi zisizo za kawaida, akitoa matamko yenye utata katika masuala mengi ya ndani na ya kimataifa. Amevuruga utaratibu wa kimataifa, hasa katika biashara, mfumo ambao Marekani ilijenga baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Miongoni mwa hatua zake ni kuzindua upya vita vya ushuru dhidi ya dunia nzima, akitaja mnamo 2 Aprili 2025 kwamba ataweka ushuru wa forodha kwa bidhaa kutoka nchi na maeneo 185. Akilenga hasa China, alitangaza ushuru wa asilimia 145 dhidi ya bidhaa zake, hatua iliyojibiwa na ushuru wa asilimia 125 uliowekwa na Beijing dhidi ya bidhaa za Marekani. Hata hivyo, baadaye Trump aliamuru kusitishwa kwa muda wa siku 90 utekelezaji wa ushuru huo kwa nchi nyingine isipokuwa China.
Katika sera yake ya "Marekani Kwanza," Trump pia alipunguza misaada ya kigeni kwa baadhi ya nchi na mashirika, akisisitiza kuwa tathmini za kina zifanywe kuhusu uhusiano wa misaada hiyo na vipaumbele vya sera ya nje ya Marekani.

Aliwadhalilisha washirika wa NATO na, kwa nia ya kutekeleza ahadi yake ya kumaliza vita vya Ukraine, alikuwa tayari kutoa nafasi kubwa kwa Russia, hatua iliyopingwa na Ukraine. Hata hivyo, baadaye katika mazishi ya Papa Francis huko Roma, Trump alikutana ana kwa ana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, na kutangaza makubaliano ya kuendeleza mazungumzo ya amani.
Wakati wa uchaguzi wa rais wa 2024, Trump alitoa ahadi mara kwa mara ya kurejesha amani duniani. Hata hivyo, hajafanikiwa katika hili hadi sasa. Licha ya kuwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa amekubali usitishaji vita huko Gaza wakati Trump aliporejea Ikulu ya White House; lakini makubaliano hayo yalikiukwa, na moto wa vita ukawaka tena huko Gaza.
Huko Ulaya, Trump ameweza kupunguza mvutano kati ya Russia na Marekani kwa kiwango ambacho kinachukuliwa kuwa mabadiliko ya kimsingi ikilinganishwa na sera ya Biden. Lakini bado hajawezekana kufikia usitishaji vita wa Ukraine, na kuna vikwazo vikubwa njiani, vikiwemo upinzani wa nchi za Ulaya na Ukraine dhidi ya mapendekezo ya makubaliano ya amani ya Trump, ambayo yangekabidhi asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine kwa Russia.
Trump pia ameanzisha mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja na Iran. Ingawa Trump alishindwa katika masuala mawili ya awali, kufikia makubaliano na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia kunaweza kuwa mafanikio makubwa kwake. Uchina, kama kipaumbele cha juu cha Marekani ulimwenguni, pia ilikuwa moja ya maeneo muhimu ya utekelezaji wa Trump katika siku mia za kwanza za muhula wake mpya.
Inaonekana kwamba, Trump bado yuko mwanzoni mwa njia ya changamoto za ndani na nje. Wakati Wademokrat wakiwa bado wamegawanyika kuhusu jinsi ya kukabiliana na Trump, hatua za Trump ndani ya nchi zimezua vita vya kisheria kati ya utawala kwa upande mmoja na baadhi ya majimbo na hata baadhi ya majaji wa mahakama ya shirikisho kwa upande mwingine.
Zaidi ya hayo, umaarufu wake uko katika kiwango cha chini sana. Kulingana na uchunguzi wa maoni, watu hawajaridhishwa na utendaji wa kiuchumi wa Trump, na hii itaongeza shinikizo kwake. Katika uga wa sera za kigeni, inatia shaka pia kwamba ataweza kupata mafanikio makubwa katika kukabiliana na migogoro na vita vya kikanda, pamoja na makabiliano ya kibiashara na China.